BARAKA ZA WAZAZI KWAKO.
Bwana Yesu asifiwe…
“….Mwaka fulani nilikuwa nikipiga stori na marafiki zangu tukiwa katika gari. Mmoja wao alikuwa ni binti naye akawa akisema yeye kamwe hawezi kufuata ushauri wowote wa baba wala mama yake mzazi kwa sababu hawajaokoka na yeye ndie ameokoka katika familia yao. Mimi sikumshangaa sana,kwa kuwa nilijua hafahamu kwamba wazazi wake wamebeba baraka zake. Hakujua kile kitendo cha kuwa mzazi tu,ni nafasi ya juu kuliko vile alivyokuwa anafikilia….”
Labda inawezekana mawazo ya namna hii na wewe unayo. Lakini ngoja tujifunze jambo hili;
Leo nataka nikutazamishe jambo hili kwa mtazamo mwingine ambao wengi wameusukumia mbali. Ukumbuke ya kwamba hata wewe unahitaji baraka za wazazi wako!
Baraka ni nguvu hai ya Kiungu iletayo mafanikio. Nguvu ya namna hii imeambatanishwa na wazazi wako. Mzazi ni yule aliyekuzaa kimwili au kiroho. Na leo tunazungumzia wazazi wa kimwili waliokuzaa,au walezi waliokulea tokeo utoto wako. Mungu ameshirikisha uumbaji kwa wanadamu katika kuzaa na kuzaa watu wengine.
Kuna nguvu katika vinywa vya wazazi/walezi pale wanapokutamkia neno. Ikiwa watakutamkia mabaya yenye sababu basi ujue yatakupata,na ikiwa watakutamkia baraka ujue zitakupata tu. Baraka zitokazo kwa wazazi wako haziangalii wokovu wao,kwa maana hata kama hawajaokoka bado wanaweza kukubariki. Unaweza kuniambia kivipi?
Jifunze kwa Labani ambaye alikuwa mzazi wa Lea na Raheli. Biblia inaeleza jambo hili kwa uwazi kabisa kuonesha baba/mama mzazi ana nguvu ya kubariki watoto wake hata kama huyo mzazi ni muabudu miungu mingine. Labani alikuwa muabudu miungu,leo tungelisema hajaokoka mtu wa namna hiyo lakini aliwabariki wanawe akina Lea na Raheli na watoto wake.
“ Labani akaondoka asubuhi na mapema, akawabusu wanawe na binti zake, akawabariki; kisha Labani akaenda zake, akarudi kwao.” Mwanzo 31:55
Labani alitamka neno kwa mabinti zake,na matamko hayo yakawa ni nguvu iletayo mafanikio kwenye siku za maisha yao. Kwa kila mzazi amepewa nguvu ya kubariki mtoto/watoto wake. Suala la kuokoka litamuhukumu mzazi yeye na Mungu wake lakini baraka zitamfikia mtoto/watoto.
Mfano wa baraka alizoziachilia Labani kwa watoto wake,suala hili ni gumu kidogo katika jamii ya leo iliyochanganyikiwa na itikadi za kiimani. Kwa maana mtu aliyeokoka leo amejijengea kwenye fikra zake kwamba mzazi wake hawezi kumbariki kama mzazi hajaokoka. Ukimuangalia Yakobo,tunaweza kumfananisha na mtu mmoja aliyeokoka leo;lakini haikumsumbua Yakobo kumpokea Labani,ili Labani aachilie baraka kwa watoto wake Lea na Raheli ambao ni wake za Yakobo.
Ni nani anayeweza kumbariki mwingine?
Mkubwa ndiye humbariki mdogo. Na hii ndio kanuni ya kipekee ya baraka. “ Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa.” Waebrania 7:7. Anayestahili kukubariki wewe ni mzazi wako (ingawa na wewe unaweza kumbariki baraka,lakini mkondo rasmi wa baraka huanza kwa mkubwa kwenda kwa mdogo)
Watu wengi leo wanapitia katika maangaiko ya hapa na pale,kwa sababu walikosa matamko ya baraka za wazazi wao. Nimeshuhudia kuona watu wakitoka majumbani na kwenda kujitegemea wakiwa hawahitaji hata wazazi kujua wanapoishi,au wengine wamewabeza wazazi wao. Kumbuka hili,hata kama umekuwa mkubwa jinsi gani lakini bado ni mtoto tu kwa wazazi/walezi wako.
Mzazi ni mzazi tu hata kama awe anachongo!
Wapo watu ambao wanawachukia wazazi wao kwa sababu wazazi wao hawajasoma kama wao. Wengine wanamchukia baba yao kwa sababu hakuwalea,labda baba yako alikutelekeza ulipozaliwa hatimaye ukajikuta unalelewa na mama kiasi kwamba umekuwa mkubwa na baba yako humjui. Sasa hata kama hali yako iko hivyo,lakini huwezi kumkataa baba yako kwa kigezo hicho,baba yako atabaki kuwa baba tu,awe amekulea au hajakulea.
Mama yako ni mama tu,umuheshimu huyo,maana bila yeye wewe usingelizaliwa. Amekulea kwa shida sana. Sasa ili upokee baraka kutoka kwao,wafanyie kitu chema wangali wa hai. Walezi wako waliokulea,watendee mema wangali wa hai ingawa huwezi kulipa thamani ya malezi yao. Hata hivyo ukionesha kuwajali hivyo hivyo jinsi walivyo.
Mambo muhimu ya kufanya;
- Wazazi wakutamkie baraka na sio laana.
- Waheshimu baba na mama yako upate baraka maishani mwako.
01. Mzazi watamkie watoto wako baraka na sio laana.
“ Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.” Waefeso 6:4
Biblia imeanza kwa kuweka mkazo mkubwa kwako mzazi kwa kuwa unawajibu mkubwa wa kuhakikisha ya kwamba unawalea vyema watoto wako katika njia ya Bwana kila siku. Waswahili husema “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”. Ukimlea mtoto vyema atakuwa katika mema,lakini ukimwacha aende mwenyewe atapotea,unamuhitaji Mungu akusaidie katika malezi yako. Tena huwezi kumlea mtoto wako katika njia ya Bwana ikiwa wewe mwenyewe haupo katika njia ya Bwana,hivyo utagundua kwamba unayo kazi kubwa. Kwanza wewe mwenyewe kuhakikisha upo vizuri na Bwana.
Kwa kuwa wewe mzazi umepewa nguvu ya kubariki watoto wako,basi hakikisha unatumia vizuri nguvu hiyo ili kusudi ilete mafanikio mazuri kwa watoto wako. Jiwekee tabia ya kuwabariki vijana/watoto wako mara kwa mara,tena kamwe usitamke laana kwao. Kwani kuna faida gani kuona kwamba watoto wako wakiangamia kwa sababu ya laana zako?. Maana kuna wazazi wanawawaambia watoto wao laana kila kukicha;mmoja wa mzazi alikuwa akimwambia mwanawe wa kuzaa “…tazama,lione kwanza,kichwa kama samaki...” Wakati mwingine husema “…lione kwanza,kichwa kama mbwa…”
Hakujua ni nguvu gani mzazi aliyokuwa nayo,kwa maana watoto wakakuwa katika laana hizo. Mmoja akafanana fanana na samaki,mwingine akachukua tabia za mbwa (tabia za umalaya,kama roho ). Sasa kuna faida gani kuona watoto wako wakiishi hivyo? Tujifunze kwa mzee Yakobo ( Mwanzo 49 yote). Yakobo akiwatamkia baraka wanawe.
02.Waheshimu baba yako na mama yako,ubarikiwe.
Kitendo tu cha kuwaheshimu wazazi wako ni baraka tosha kwako. Kuna mambo yako mengine yamefungwa kwa sababu hujawaheshimu wazazi wako. Unajua si kila kitu ni shetani,mambo mengibe ni wewe mwenyewe umesababisha kushindwa kuziona baraka zako. Jiulize kwako,je wewe ni mtiifu kwa baba na mama yako? Usiniambie kwamba wazazi/walezi wako ni wakolofi au ni wabaya,bali unawaheshimu inavyostahili? Biblia inasema;
“Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.” Waefeso 6:2-3
Amri ya kwanza yenye ahadi ni hii tu,ya kumuheshimu baba na mama yako. Ahadi hii ni kupokea baraka na kukaa siku nyingi katika dunia. Leo kuna shida sana katika hili eneo,kiasi kwamba watu hawaoni baraka zao wakidhania ya kuwa shetani amezuilia. Mfano mdogo ni huu; utakuta mtu kweli kaokoka lakini ameelekeza kuwajali watumishi wa kiroho zaidi kuliko baba na mama yake mzazi.,akiambiwa kwamba atoe pesa kwao haoni shida na hutoa mara moja lakini akiambiwa na baba/mama yake atoe pesa hanasema “ mama mimi sina”
Sasa huwezi ukabarikiwa kwa namna hiyo hata kidogo. Emu angalia mfano huu
baba wa kiroho anamwambia binti yake anayemchunga “ mwanangu jitahidi kuninunulia viatu mwezi huu,ninunulie na suti nzuri za kama laki 5 hivi au 4 kama ukipungukiwa,usisahau na pesa kidogo ya kuweka mafuta ya gari yangu...” binti naye anapokea kwa sababu ameambiwa na baba yake wa kiroho ambaye humbariki na ni vyema kabisa. Lakini papo hapo huyo binti ajawahi kumnunulia mama yake mzazi hata dela la elfu 13 ampelekee!!! Hajawahi kumnunulia mzee wake aliyopo kijijini hata shati la elfu 15 ampelekee. Sasa huyu binti Je anawaheshimu wazazi wake kweli? Kama lah hawaheshimu!!! Atapokeaje baraka???
Si vibaya hata kidogo kuwavalisha watumishi wa Mungu kama mimi ninayekuandikia hapa,lakini ni vibaya pale unapowavalisha alafu wazazi/walezi wako unapowasahau!!! Ingependeza uanze na wazazi waliokuzaa na kukulea tokea upo mtoto mchanga usiyejitambua hata sasa,ndiposa uwavalishe wapakwa mafuta wa Bwana. Kumbuka hili “ Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.” 1 Timotheo 5:8
Ukiwa kama uliondoka kwenu bila kupokea baraka za wazee,sasa chukua hatua hurudi kwa toba ili Mungu akusamehe na wazee wako pia wakuachilie,kisha wakubariki kule uendako. Ujumbe huu ni wa kwako siku ya leo,Mungu anataka akubariki zaidi lakini kwanza utengeneze na wazee wako.
Na ikiwa kwako imekuwa ni vigumu,labda wazee walishakufa wote nawe uliondoko pasipo amani. Au hujui sasa ni nini cha kufanya,naomba unipigie simu sasa;usisite piga kwa 0672870833UBARIKIWE.
Post a Comment