HATUA NANE(8) ZA KWANZA ZA USHINDI KATIKA VITA YA KIROHO
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ni kweli kabisa maombi ni silaha namba moja ya kumshinda shetani na wapambe wake, lakini ROHO wa MUNGU siku moja akanijulisha mambo nane muhimu ya kwanza kabisa ya ushindi katika vita ya kiroho, mambo haya nane yakiambatana sambamba na maombi ushindi wake ni mkuu sana.
Lakini pia katika maombi yako wakati mwingine ukipewa maelekezo rohoni mwako yanayoambatana na maombi hayo zingatia maelekezo hayo, wakati mwingine rohoni mwako katika maombi unaweza kuelekezwa nadhiri, sadaka n.k
Maelekezo hayo kama kweli umefunuliwa rohoni mwako bila shinikizo la mtu basi zingatia sana.
Vita ya kiroho ni nini?
Vita ya kiroho ni mapigano ya kiroho baina ya ulimwengu wa roho wa Nuru na ulimwengu wa roho wa giza.
Ni vita baina ya mwanadamu na nguvu za giza.
Mwanadamu aliumbwa na MUNGU katika ulimwengu wa roho wa nuru lakini shetani ameshawafanya baadhi ya watu kuhamia ulimwengu wa roho wa giza na kuwa kinyume kabisa na watu wa MUNGU walio katika ulimwengu wa roho wa nuru.
Katika maisha yako una vita na hiyo vita inatoka ulimwengu wa roho wa giza.
Waefeso 6:11 ''Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani ''
Katika ulimwengu wa roho wa giza kuna madhabahu za giza, wachawi, waganga wa kienyeji, majini, mizimu, wakuu wa giza na wanadamu wanaotumika kipepo.
Katika kushinda vita ya kiroho unahitaji sana kuwa muombaji lakini maombi yako lazima yaambatane na mambo haya manane ndipo utashinda kirahisi.
Wako watu wako katika vita kubwa sana ya kiroho.
Ngoja nikupe mifano hai kabisa juu ya mtu kujikuta katika vita kubwa ya kiroho.
Mama mmoja alipokuwa mimba alitafuta msichana wa kazi mdogo tu kiumri, lakini msichana yule kumbe alikuwa anatumia madawa ya kiganga, baada ya miezi michache tu tangu awe kwenye familia hiyo alianza kutembea na baba wa familia, baadae kidogo tu yule baba alibadilika na kutaka kumfukuza mkewe akiwa mimba karibu na kujifungua. Baba yule akatangaza kwamba mke wake sasa ni yule House girl na yule House girl alimuweka wazi yule mama kwamba sasa hana chake tena na kumtukana sana na ikafika kipindi mama mwenye nyumba ndio akawa kama house girl na house girl halisi akawa ndio mama mwenye nyumba. Baba wa familia alikuwa na mshahara mkubwa lakini hata mia hakumpa mkewe ila house girl ndio alikuwa anamiliki ATM Card. Vita ya kiroho ya mama yule ili kuirudisha ndoa yake ni vita kubwa sana, lakini Ukijua hatua za ushindi katika vita vya kiroho hakika utashinda.
Mama mmoja siku anafunga ndoa kuna mtu anayetumika kipepo alimpa zawadi ikiwa na maagano mabaya ya kipepo ya kumzuia kuzaa, mtoa zawadi alitoa zawadi huku anacheka na kupita kigelegele lakini akamsogolea bi harusi kwa mbwembwe na kumwambia ''Ikitokea hutazaa utafanyaje'' . Bibi harusi yule alidhani ni matani na hakujua kwamba shetani ameshafanya yake, Bila ufunuo wa ROHO MTAKATIFU hakika angeweza kuwa tasa miaka yote.
Baba mmoja alikuwa anafanya ngono na majini ndotoni bila kujua kwamba kuna madhara mbele yake. Alipokuja kufunga ndoa uzao ulikosekana katika ndoa yake, alijaribu kila dawa na ushauri lakini haikuwezekana, alianza kuombewa kwa muda hadi alipokuja kufunuliwa kwamba majini yale yalichukua mbegu zake za kiume na kwenda kuzizika katika milima mirefu mitatu duniani na kutoa karafa ili kumzuilia uzao. Vita ile ya kiroho ilikuwa kubwa sana na ngumu hadi ufunuo wa ROHO ulipotokea ndipo akaharibu kazi za giza na kushinda.
Mama mmoja aliugua ghafla magonjwa ya ajabu sana ambayo hata kwenye vipimo hospitalini ugonjwa wowote haukuonekana. Mama yule baada ya mombezi kidogo aliona hatapona kwa maombi hivyo akaenda kwa mganga wa kienyeji na akafia huko. Kumbuka aliyeuleta ugonjwa ni wakala wa shetani, na ukienda kwa wakala wa shetani ujue unaenda kumalizikia. Lakini kwanini mtu kama huyu ashindwe katika vita ya kiroho?
Ni kwa sababu hajui hatua za ki MUNGU za ushindi katika vita ya kiroho.
Leo kuna maelfu ya watu wanaenda kupona na baada ya kuzishika hatua hizi nane za ushindi katika vita ya kiroho, ili wakiomba tu wafanikiwe kwa jina la YESU KRISTO.
Hatua 8 za kwanza za ushindi katika vita ya kiroho.
1. Zijue mamlaka 4 za Mteule wa KRISTO na uzitumie mamlaka hizo katika maombi.
Mamlaka hizo nne za mteule wa MUNGU ni;
A. Jina la YESU KRISTO.
Yohana 14:14 ''Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.''
Ili ushinde ni lazima ujue kulitumia jina la YESU KRISTO katika maombi yako, na jina la YESU KRISTO, sio wote wanajua kulitumia jina la YESU KRISTO.
Wengine hulitumia jina la YESU kama kwa kujifurahisha tu na sio kwa imani.
B. Damu ya YESU KRISTO
Ufunuo 12:11 '' Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.''
Ili ushinde ni lazima ujue kuitumia damu ya YESU KRISTO ambazo hakuna kitu ambacho haiwezi kufuta, hakuna agano la giza ambalo damu ya YESU haiwezi kufuta.
C. Nguvu za ROHO MTAKATIFU.
1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU"
Lazima ujue kuzitumia nguvu za ROHO MTAKATIFU, Nguvu za ROHO MTAKATIFU zinaweza kushuka na ufunuo wa ROHO MTAKATIFU au Neno la Ufunuo la kukusaidia kushinda.
Nguvu za ROHO MTAKATIFU ni ulinzi wako. Kwenye nguvu za ROHO MTAKATIFU mchawi wala jini hawezi kufika hapo.
D. Neno la MUNGU
Zaburi 107:20 '' Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. ''
Neno la ufunuo la MUNGU hukuonyesha nini cha kufanya, Neno la MUNGU hukuongezea imani na Neno la MUNGU huwatisha mawakala wa shetani wote.
Ili ushinde ni muhimu kujua mamlaka za Mteule wa MUNGU ambazo kwa hizo hakuna wakala wa shetani anaweza kukushinda.
Hizo mamlaka nne za mteule wa MUNGU nimeshawahi kuzifafanua katika somo zima hivyo leo sijazizungumzia sana maana hili ni somo lingine.
2. Usikubali kutenganishwa na MUNGU kwa namna yeyote.
Ayubu 19:25 '' Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.''
Kazi mojawapo ya mawakala wa shetani ni kukutenganisha wewe na MUNGU. Ukiona mtu anaenda kwa mganga ni kwa sababu shetani amemdanganya na uongo huo umetenganisha mtu huyo na MUNGU Baba wa mbinguni.
Ukiona mtu hawezi kusamehe, anachukia watu, anafanya dhambi au analipiza kisasi kimwili, hizo zote ni kamba za shetani ili kumtenganisha mtu huyo na MUNGU.
Andiko hapo juu linamuonyesha Ayubu aliyekuwa katika vita kubwa zaidi ya kiroho lakini alijua moja ya kosa kubwa ni yeye kujitenga mbali na MUNGU hivyo aling'ang'ania Kwa MUNGU wakati wote. Ndugu ili ushinde vita ya kiroho usikubali kutenganishwa na Bwana YESU kwa namna yeyote, usikubali kutenganishwa na MUNGU kwa namna yeyote.
Wengi tunaowaombea wakati mwingine unakuta uhusiano wao na MUNGU ulishavunjika siku nyingi. Ndugu ukikubali kutenganishwa na Bwana YESU hakika ukijitenga naye huwezi tena kushinda vita ya kiroho. Kama unataka kushinda vita ya kiroho uliyonayo hakikisha uko pamoja na MUNGU Baba kupitia YESU KRISTO Mwokozi.
Ayubu angekubali ushauri wa mke wake au wa marafiki zake ili ajitenge mbali na MUNGU hakika angekufa siku hiyo hiyo, ndugu ukitaka kushinda vita ya kiroho usikubali kutenganishwa na YAHWEH MUNGU kwa vyovyote, wengi kwa sababu ya vita ya kiroho hutukana watumishi wa MUNGU na kujiongezea laana, wengi huacha ibada na huacha maombi na hujinajisi kwa mambo mengi na ndio maana hawajashinda vita ya kiroho.
3. Usikubali kutoa siri zako kwa kila mtu.
Waamuzi 16:16-18 '' Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa. Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa MUNGU, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.''
Kitendo cha Samsoni kutoa siri kwa Delila kulisababisha Samsoni atobolewe macho, aondolewe nguvu zake, awatumikie maadui zake wafilisti.
Ukiwa katika vita ya kiroho ni muhimu sana ukajua aina ya vita uliyonayo na maadui unaopambana nao. Kuna wengine wakijua siri zako ndio mwanzo wa kukumaliza. Sina maana ya kwamba usitoe kabisa siri zako lakini mimi nakushauri siri zako waeleze watumishi wa MUNGU ambao watakuombea na sio kumweleza kila mtu.
Binti mmoja vita yake ilikuwa ni jinsi ya kupata mchumba, baadae alipata mchumba lakini hata huyo mchumba akachukuliwa na rafiki yake siku chache kabla ya ndoa, kwa sababu tu rafiki huyo alikuwa anajua kila siri kuhusu uchumba huo. Unaweza kuwa unarogwa na wewe kila siku unamwambia mchawi jinsi unavyoumwa na jinsi unavyosikia maumivu na mchawi huyo anajipongeza kimoyomoyo huku akipanga kukuongezea magonjwa. Sio watu wote ni watu wazuri kwako. Katika nyakati hii hata rafiki wa karibu naweza kuwa wakala wa shetani ili kukuangamiza. Katika vita ya kiroho hakikisha siri zako unawaeleza wachungaji tu na watumishi wa MUNGU waaminifu. Unaweza kuwa una vita kazini kwako na unataka kufukuzwa kazi, wewe huwa unamweleza rafiki yako kila mchakato na kumbe huyo ndie aliye nyuma ya wewe kufukuzwa kazi, vita ya kiroho ya hivyo unaweza ukafeli kila siku kwa sababu tu unatoa sirib kila siku kwa watu wasio sahihi.
4. Usikubali kuruhusu uoga na hofu vikaingia ndani yako.
Zaburi 56:4 '' Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Nimemtumaini MUNGU, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini?''
Woga na hofu ni moja ya silaha za shetani kukushinda wewe kirahisi.
Ili ushinde vita ya kiroho hakikisha huna hofu wa uoga.
Wengine ni waombaji lakini wamejaa hofu na woga ndio maana hawajibiwi maombi yao.
Kuna mtu akisikia tu paka wanalia nje ya nyumba anaweza hata akahama nyumba ile. Wewe kama una YESU KRISTO Mwokozi hakikisha hofu mashaka na uogo sio sehemu ya maisha yako. Ukiwa huna hofu wala uoga hakika mawakala za shetani wanaweza kukimbia mbele yako hata kabla hujaomba.
5. Ondoa mitego ya shetani kwa umakini.
1 Petro 5:8'' Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.''
Ili shetani akukimbie unatakiwa umtii MUNGU huku ukimpinga huyo shetani ndipo atakukimbia, akikukimbia shetani umeshinda vita ya kiroho.
Kuna mitego ya giza unatakiwa kuiondoa kwa umakini na maadui zako watashangaa tu kila wanalolipanga halifanikiwi.
Mama Mchungaji mmoja aliniambia kwamba siku moja aliota ndoto kanisani kwao kuna mtu anaenda jioni moja kuchimbia kibuyu ili kanisa lisambaratike, alipoona maono hayo alimshilikisha Mchungaji na walipokwenda kanisani kuna mtoto mdogo alimuona live yule Mchawi akichimbia kibuyu pembeni ya Kanisa, akawaonyesha na wakakitoa kile kibuyu. Kibuyu hicho ni mfano wa mtego wa shetani ambao unatakiwa kuuondoa.
Mama mmoja alipewa chakula na jirani yake kwenye bakuli, alipokuwa anaondoka na chakula hicho ambacho kimepikwa aliona vita rohoni na hakukila chakula kile, alichokifanya alifika akamwaga kwenye chombo chake cha takataka na kwenda kumwaga, yule aliyempa anayetumika kipepo aliulizia utamu wa chakula kile akaambiwa ni kitamu, akafurahi na kusubiri madhara lakini hakuyaona hata siku moja hadi akashtuka. Kumbe mtego wake uligunguliwa na kuharibiwa zamani.
Mitego ya shetani iko mingi sana hakikisha unaiondoa yote kwa umakini, mitego inaweza kuwa kwenye zawadi, chakula, nguo, kwenye kiti cha ofisi yako, kwenye bishara yako au popote.
6. Mtumaini MUNGU siku zote.
Mithali 3:5-6 ''Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. ''
Ndugu mmoja aliniambia kwamba nimuombee ili apate Mchumba lakini akasema tena kwamba yeye Binafsi hawezi tena kuombea jambo hilo maana ameshaliombea siku nyingi sana. Nilimshangaa lakini nikagundua kwamba ndugu huyo kwa sasa hamwamini MUNGU ndio maana hawezi kumuomba tena juu ya hitaji hilo.
Ukitaka ushinde vita ya kiroho hakikisha unamtumaini MUNGU siku zote.
Wengi sasa wanatumaini akili zao wenyewe na sio MUNGU ndio maana wanashindwa katika vita ya kiroho.
Ndugu, ukitaka ushinde katika vita ya kiroho hakikisha unamtumaini MUNGU. Kwenye suala la kumtumaini MUNGU hakikisha akili zako hazihusiki.
Njia mojawapo ya kukuonyesha kwamba unamtumaini MUNGU ni pale ambapo unamkiri YESU kama Mshindi wako, unakiri hata mbele za watu kwamba MUNGU atakushindia.
Ukitaka ushinde vita ya kiroho hatua ya kwamba muhimu sana ni wewe kumtumaini MUNGU siku zote.
7. Enenda kwa ROHO MTAKATIFU.
Yuda 1:20 ''Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU, ''
Kuenenda katika ROHO MTAKATIFU kunahusisha pia kuomba katika ROHO MTAKATIFU na kumsikiliza ROHO MTAKATIFU huku ukimtii yeye.
Kumbuka ROHO MTAKATIFU hufumbua mafumbo yote '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU-1 Kor 2:10 "
ROHO MTAKATIFU huliona jambo mwisho kabla ya mwanzo hivyo anapokushauri au kukuelekeza hakikisha unamtii maana yeye hakosei.
Ukitaka kushinda vita ya kiroho hakika hakuna kama ROHO MTAKATIFU kwako.
ROHO MTAKATIFU anaweza akakujulisha kila siri kutoka ulimwengu wa roho, anaweza akakufundisha njia za kushinda na anaweza akakuondoa eneo baya kwako au anaweza akakupa mbinu za kiroho za kushinda kirahisi sana.
Mhitaji sana ROHO MTAKATIFU na Mtii yeye kama kweli unataka kushinda vita ya kiroho.
8. Weka msingi wako wa ushindi kwenye Neno la MUNGU.
Zaburi 12:6 '' Maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.''
Wengi sana wanafeli katika vita ya kiroho kwa sababu wameweka msingi wao kwa watumishi.
Wengi sana wamefeli vita ya kiroho kwa sababu wameweka msingi wao kwenye vitu, mfano mafuta ya upako, chumvi, sanamu za akina Mariamu, viti au vitu vingine vyovyote.
Ndugu ukitaka kushinda vita ya kiroho hatua ya kwanza kabisa weka msingi katika Neno la MUNGU.
Ukiweka msingi kwenye mafuta ya upako au sanamu unayodhani ni ya Yesu ujue utaaanza kuamini zaidi vitu hivyo kuliko MUNGU.
Ukiweka msingi wako wa uponyaji kwa mtumishi utaanza kumwamini Mtumishi huyo kuliko ROHO MTAKATIFU au kuliko MUNGU mwenyewe.
Ndugu, ukitaka kushinda vita ya kiroho hakikisha unaweza msingi wako wa ushindi katika Neno la MUNGU.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako EV.MCHOME
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0 672870833(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji na hadi
Home > ROHO MTAKATIFU > Hatua za kushinda vita vya kiroho
Hatua za kushinda vita vya kiroho
By Yote Yanawezekana Kwa Yesu • October 24, 2019 • ROHO MTAKATIFU • Comments : 6
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Nice teachings, may The living Gobbles you.
ReplyDeleteThanks be blessed always
ReplyDeleteMungu akubariki sana!!
ReplyDeleteBwana Yesu asifiwe.Mungu Baba azidi kukufunulia,ili kundi lake lipate lishe bora ya kiroho.Natamani kupata ufafanuzi wa mamlaka nne za mteule wa Mungu.Nifanyeje?
ReplyDeleteMungu akubaliki sana sana
ReplyDeleteMungu akubariki sn mtumishi
ReplyDelete