Headlines

Kufunga na kuomba

01. Nini hasa maana ya kufunga?
Kufunga ni hali ya kuutiisha mwili wako kwa kuunyima chakula pamoja na vinywaji kwa makusudi ili upate muda mzuri wa kusema na Bwana,kwa muda maalumu. Ikiwa utaunyima mwili chakula,ni dhahili utahisi uchovu wa kawaida,lakini hapo ndipo roho yako ipate kusema na Bwana. Utagundua,kufunga ni aina fulani ya mateso ya makusudi dhidi ya mwili,lakini ni mateso yenye matokeo mazuri.“Magoti yangu yamedhoofu kwa kufunga,Na mwili wangu umekonda kwa kukosa mafuta.”Zaburi 109:24. Pia Zab.35:13c “… Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga;…”
Mwili ukikosa chakula kwa muda mrefu,hapo mwili hukosa mafuta na kwa sababu hiyo kukonda kunaweza kuonekana kama dalili. Hata hivyo,haina maana kwamba kila atakayefunga atakonda,la hasha! kama kukitokea kukonda,basi huwa ni kwa muda tu,lakini mara nyingi hatukondi badala yake tunanawili hali tukiwa tumefunga. Kumbuka;mwenye kufunga ni yule aliyefunga mizunguko isiyoyalazima,bali muda wake amewekeza kwa Bwana. Hivyo utagundua kwamba kufunga ni moja ya tendo kubwa sana la imani. Kwa maana kwenye kufunga ``imani ” ndio msingi mkubwa. Na ndio maana asiyekuwa na imani hawezi kufunga. Hivi juzi juzi nilikuwa na rafiki zangu wazungu fulani ambao wao hawaoni umuhimu wowote wa kufunga kwa sababu nyingi walizonazo,tamaduni zao baadhi yao wanaona shidi kutesa miili yao! Kwa kweli mtu mwenye imani kwa Kristo Yesu na hafungi,lazima atakuwa na matatizo tu.
02. Kwa nini tunafunga?
  • Kwa sababu tunajifunza kwa Yesu. – Yesu naye alifunga ( Mathayo 4:1-2), Ingawa Yesu alifunga siku 40 mchana na usiku,sisi tunaweza kufunga kwa kadiri atuwezeshavyo Roho mtakatifu. Kama kufunga kusingelikuwa na maana basi sidhani kama Yesu angelifunga. Kila alichokifanya Yesu kilikuwa na maana kubwa sana,na ndio maana anasema “ …mjifunze kwangu…” Mathayo 11:29.. Ikumbukwe wazi kwamba,Yesu alikuwa mwanadamu 100% na Mungu %,Na anataka kuona kila mfuasi / follower of Christ,anafanya kile alichofanya.
  • Kuna mambo yasiyotoka,mpaka kufunga na kuomba.- Ingawa wapo watu wanaopinga ukweli huu,lakini ndio ukweli halisia,kwamba kuna mambo mengine yanahitaji kujitoa kwako katika kumtafuta Bwana ndio yapatikanike.  Na kuna mengine hayawezekani mpaka utakapotia ufahamu wa kufunga na kuomba“ [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]” Mathayo 17:21
Tafsiri halisi ya andiko hili ni kufunga na kuomba kama mchakato mzima wa maisha ya mwanadamu. Hapa hapana maana kwamba ufunge kwa mambo magumu tu,bali ufunge mara kwa mara kwa sababu ni moja ya msingi wa imani yetu. Neno la Mungu linatutaka tuwe na maombi na mfungo endelevu kama nguzo/msingi wa imani yetu.  Haya mawili “kufunga” na “kuomba” yanakwenda pamoja,ni mapacha.
Kwa maana mtu mwombaji anapaswa awe mfungaji. Yeye aombaye mara kwa mara bila kufunga hapokei majibu yote kwa maana ameacha kufunga kama utaratibu tena mengine hayatoki namna hii bila kufunga nakuomba. Naye vivyo hivyo yeye afungaye pasipo maombi basi funga yake hukosa nguvu kwa sababu hakuomba wakati wa kufunga.
03. Kufunga kulianzia wapi?
Kufunga kulianzia muda mrefu,tangu enzi hizo kabla ya ujio wa Yesu. Wapo baadhi ya waamini waliokuwa wamekaza kwa Bwana wakijua nini hasa maana ya kufunga na kuomba,nao walifunga. Na tunashuhudia mtokeo ya watu waliofunga. Hata hivyo,hali haikuwa kama ya sasa kwa maana watu walitumia njia ya kufunga pale walioutafuta uso wa Bwana hasa kwa mambo magumu yaliyoshindikanika. Ebu tazama mfano wa watu wa Yuda chini ya Yehoshafati ;
walipoinukiwa na mataifa matatu yenye nguvu ( waliinukiwa na wana wa Moabu,na wana wa Amoni na wana wa Wameuni. Lakini Yehoshafati akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote – 2 Nyakati 20:1-3). Na mwishoe akina Yehoshafati wakaibuka washindi. Lakini ukichunguza kilichowafanya waibuke washindi wa vita ni ile hali ya kumtafuta Bwana Mungu kwa njia ya kufunga na kuomba.Katika agano jipya,“ kufunga na kuomba” ni mazoezi ya kujenga misuli ya imani. Kuanzia kwa Yesu mpaka mitume walitumia muda wao kujijenga kwenye misuri ya imani. Ilikuwa ni kuutafuta uso wa Bwana kwa bidii yote. Tunawaona wengi wakifunga lakini waliomba pia katika Jina la Yesu Kristo.
04.Aina za kufunga.
Biblia haijaweka aina mbali mbali za kufunga,isipokuwa tunaweza kujifunza aina hizi kwa kujifunza kwa wale waliofunga. Wakati ninalichunguza jambo hili,nikagundua aina tatu ambazo tunaweza kuzitumia siku za leo;
i)Kwa masaa 12 ya siku.
Wengi hufunga kwa masaa 12 ya siku hasa saa za asubuhi,mchana na jioni kufungulia. Mtu akifunga kwa masaa ya siku,huwa tunasema kafunga siku moja. Hata hivyo wengine wamekosa muda wa maombi,sasa hawawezi kufunga huku wamekosa muda wa maombi kwa sababu ya kazi za kutwa. Hivyo,baadhi yao wamejiwekea taratibu za kuwa na maombi usiku kuanzia jioni. Kitu ambacho si vibaya pia. Cha muhimu ni kuomba na kufunga.  ( Luka 2:36-37)
ii) Tatu kavu.
Ni mfungo wa kutokula wala kunywa muda wa siku tatu. Dhima kubwa ya mfungo wa namna hii ni kwa ajili ya mambo makubwa,magumu yasiyowezekana katika hali ya kawaida.Ukweli ni kwamba hatufungi ili kumlazimisha Mungu ajibu,HAPANA!!! Bali kwa imani,tunapofunga Mungu hutusaidia akiangalia kiu,na shauku tuliyonayo,akijibu kwa wakati wake. “ Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.” Esta 4:16. Esta hakumlazimisha Mungu ajibiwe,bali alifanya kwa upande wake kile awezacho! ( Soma pia Matendo 9:9)
iii) Siku 21. (Danieli 10:2-3),Siku 40 ( Kutoka 34:28,1 Wafalme 19:8) Pamoja na siku saba.
  • Swaumu aliyoichagua Bwana (Isaya 58:6-8)
Kuna kufunga tulikokuchagua sisi kwa malengo yetu mbali mbali,hasi kujiimarisha katika imani yetu. Lakini kuna kufunga alikokuchagua BWANA ambako kunamkazo wa mambo yafuatayo “kufungua vifungo vya uovu,kulegeza kamba za nira,kuwaacha huru walioonewa,kuvunja nira zote,kuwapa chakula wahitaji,kuwajali maskini” na matokeo yake yatakuwa ni “utukufu wa Bwana utakufuata,na kukulinda”. Huu ndio mtihani sasa! na ndipo hapo penye kukamilisha funga yako,na hatimaye kulindwa na Bwana,tena biblia inasema utukufu wa Bwana utakufuata. Ni sawa na kusema “upako wa Bwana” hautakupungukia,utalindwa!
05.Mifano ya waliofunga;
Yesu kama kielelezo chetu,naye alifunga. Lakini kuna watumishi wengine walifunga kama vile;
  1. Esta. – Esta 4:16
  2. Musa -Kutoka 34:28
  3. Eliya mtishbi-1 Wafalme 19:8
  4. Hana mama yake Samweli. 1 Samweli 1:18
  5. Ana binti fanueli – Luka 2:36-37
  6. Danieli – Danieli 9:3,10:3
  7. Nehemia- Nehemia 1:4
  8. Watu wa Ninawi -Yona 3:5
  9. Paulo mtue –  2 Wakorintho 11:27
  10. Kanisa la kwanza huko Antiokia – Matendo 13:2-3
06. Matokeo ya kufunga;
  1. Kukujengea misuli ya imani.(Luka 4:1-2)
  2. Kutembea kwenye utukufu wa Bwana (Isaya 58:8)
  3. Kuvikwa nguvu za kiroho na upako.
  4. Kuvikwa sila zote za Mungu kwa ajili ya kuzipinga hila zote za shetani.
  5. Ni chanzo cha kupata kusikia na kuona kiroho.
07. Matokeo yanayoweza kukujia kama huna tabia ya kufunga kabisa – Kuwa kimwili sana,kiasi kwamba hata kushindwa kujua mambo ya rohoni
08. Ninawezaje kufunga?
Wapo watu wengi ambao bado hawawezi kufunga. Wengine ni kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao,kwa mfano magonjwa. Lakini wengine hawajawahi kufunga kwa sababu ya imani walizonazo huko mwanzo walikotoka kwenye dini zao,ambapo kulikuwa hakuna kufunga. Lakini ikiwa mtu hajawahi kufunga,bado hajachelewa kwa maana anaweza akaanza sasa. Na njia pekee ya kufanikiwa kufunga,ni kumwomba Roho mtakatifu akuwezeshe kwa kuitawala njaa. Yeye anaweza,kwa maana ni Yeye Roho wa Mungu aliyewawezesha wote na ndiye huyo huyo atakuwezesha na wewe pia.
Lakini kitu cha pili ni kuanza taratibu kwa masaa machache ya mwanzo,kidogo kidogo huku ukiendelea kuomba. Mazoezi ni muhimu sana. Hata hivyo,ni vyema ukawasiliana na mchungaji au mtu wa Mungu aliyepo karibu yako,akuongoze. Kumbuka; kufunga kunakuja kwa sababu ya “nia ya ndani” yaani ujiulize,unafunga kwa nia gani,kitu gani kinakusukuma ndani yako? Na je neno la Mungu linasemaje?
  • Kufunga hutembea na Neno.
Ikiwa kama utafunga,ni lazima usome neno la Mungu. Kwa maana Neno litakuongoza kwa kukupa maarifa ya namna gani uombe pia. La! Kama unafunga bila Neno,ujue kuna mahali utakwama tu,kwa sababu sio taratibu ya kufunga. Yeyote anayefunga na kuomba ni lazima awe msomaji wa Neno na mwenye “kulitafakari Neno”
Ikiwa kama umebarikiwa,nifahamishe- Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI pigia kwa simu zangu hizi 0672870833

Share this:

11 comments :

 
Copyright © Yote Yanawezekana Kwa Yesu. Designed by OddThemes