Headlines

Faida ya maombi ya kufunga

FAIDA SABA ZA MAOMBI YA KUFUNGA.

        1.     Maombi ya kufunga yanaweza kukufanya uongezeke kiimani.

Mathayo 17:21 ‘’ [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]   ‘’

-Kwa sababu kuna mambo ambayo yatawezekana tu baada ya kufunga, naamini imani yako itaongezeka kupitia matokeo ya kufunga kwako.

Mfano. Ulikuwa ukihitaji kupata kazi kwa muda mrefu sana. Uliomba maombi ya kawaida na bado hukufanikiwa kupata kazi, baada ya kuamua kufunga siku 5 ukajikuta unapata kazi na pia ukawa unapigiwa simu kwamba unahitajika katika kazi 3 tofauti. MUNGU amekujibu ombi lako la kupata kazi na nahakika imani yako itaongezeka sana. Ndio maana nasema hivi maombi ya kufunga yanaweza kusababisha imani yako ikue, hiyo ndio sifa ya kufunga na kuomba kisha kupokee kutoka kwa BWANA.

        2.     Macho yako ya ndani yatakuwa yanaona vizuri.

Zaburi 119:18 ‘’ Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako. ‘’

-Mambo mengine ya kiroho kuyajua  ni lazima ufumbuliwe macho ndipo utaona na kujua.

-Kuna vitu vingi sana ambavyo sikuwahi kuvijua wala kuviona lakini baada ya maombi ya kufunga niliona na kushangaa sana.

-Biblia inaposema kwamba ”Unifumbue macho yangu nitazame” maana yake mwanzo hakuweza kutazama  na kuelewa hata kama macho anayo ila macho ya ndani yalikuwa yamezibwa ndio maana hakuona, na katika hilo tunarudi pale pale kwamba ”Mengine yatawezekana tu baada ya kufunga na kuomba”

-Maombi ya kufunga yatafungua macho yako ya ndani na na utaona hata maadui walio sirini ambao wamekutesa kwa muda mrefu. 

.       3.   Mwili wako utakuwa umetiishwa.

Wakolosai 3:5 ‘’ Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;‘’

-Ndugu yangu, kuutiisha mwili wakati mwingine hauhitaji tu kujaribu kuishi maisha matakatifu bali ni kuishi maisha matakatifu huku ukiomba na maombi ya kufunga ndio yaliyo na nguvu zaidi za kukusaidia katika hilo.

-Unapofunga na kuomba hata kama hukuombea kutiisha mwili wako lakini lazima tu mwili wako utiishwe kutokana na maombi uliyoomba hata kama hukuombea jambo hilo. 

-Maombi ya kufunga ni tiba kuu ya vitu vinavokutesa ambavyo viko katika mwili wako.

-Kama unateswa na mwili wako kwa kuwaka tamaa ya ngono, basi funga na kuomba na mwili wako uttiishwa.

-Kama mawazo mabaya yanakutesa basi funga na kuomba yataondoka.

-Kitu chochote ambacho kinakuendesha bila hata wewe binafsi kutaka, lakini unajikuta tu ukikitii kitu hicho ambacho ni machukizo, basi funga na kuomba utashinda.

 1 Thesalonike 5:17  ”ombeni bila kukoma;”

-Njia mojawapo ya kuutiisha mwili wako hata usinaswe na dhambi wala tamaa mbaya ni kwa njia ya kufunga.

-Kama umekuwa unateswa na mawazo machafu yanayokunajisi basi ukifunga na ukaomba kweli katika kufunga kwako hakika mawazo hayo machafu yataondoka.

-Kufunga ni muhimu sana kwa wewe ambaye dhambi za zamani zinataka kukuteka tena. Funga na omba hakika utabaki mshindi daima.

 Marko 11:24 ”Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”

     4.   Kupokea maana ni ahadi ya MUNGU kujibu maombi yako.

Yeremia  29:13 ‘’Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.”  Tena Biblia inasema  ”Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;-Mathayo 7:7”   na kwa sababu MUNGU analiangalia neno lake alitimize basi hata aliposema tuombe ni hakika atajibu maana yeye hajipingi na Neno lake, labda tu sisi tuombe vibaya na tupungukiwe na imani katika maombi yetu.

1 Yohana 5:14-15 ”Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” 

-Maombi ya kufunga ni mkono mrefu wa kupokea kutoka kwa MUNGU.

 Waebrania 4:16 ”Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. ”

      5.  Utamruhusu ROHO MTAKATIFU kukutumia.

1 Kor 12:11 ‘’ lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. ‘’

-ROHO MTAKATIFU humgawia kila mtu huduma kama atakavyo yeye ROHO lakini wakati mwingine huduma unayo lakini haiendelei kwa sababu huombi ndio maana BWANA YESU akasema ” Mengine yatawezekana kwa wewe kufunga na kuomba”

 -Maombi ya kufunga ni muhimu sana na inakuwa rahisi zaidi ROHO MTAKATIFU kukutumia maana hata wewe unakuwa rohoni.

-ROHO pia anaweza kukutumia kwa maombi.

 Warumi 8:26-27 ”Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya ROHO ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo MUNGU”.

      6.   Utatumika kwa MUNGU vizuri

Matendo 13:2-3 ‘’Basi hawa walipokuwa wakimfanyia BWANA ibada na kufunga, ROHO MTAKATIFU akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.’’

-Maombi ya kufunga yalifungulia njia ya watumishi hawa kuitwa na kupewa jukumu na MUNGU.

-Hata wewe unaweza kuwa katika kufunga na MUNGU akasema na wewe jambo fulani ambalo unatakiwa ulitende, unaweza kujiuliza kwanini ROHO hakusema wakati hawakufunga na kuomba?

Maombi ya kufunga ni muhimu sana.



     7.    Utakuwa na nguvu za MUNGU.

Mathayo 11:12 ‘’Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.‘’

-Ndugu, watu wenye nguvu tu ndio wanaouteka ufalme wa MUNGU. nguvu zinazozungumzwa hapa sio nguvu za miili ila ni nguvu za rohoni ambazo hupatikana kwa kujifunza neno la kulijua, kuishi maisha matakatifu, kumtumikia BWANA YESU na kuomba sana. na maombi ya kufunga ndio maombi ambayo yatakufanya uwe na nguvu zaidi za rohoni hata shetani asikurudishe nyuma

Share this:

1 comment :

 
Copyright © Yote Yanawezekana Kwa Yesu. Designed by OddThemes