Headlines

KAZI KUU TANO ZA IMANI (UMUHIMU WA IMANI)

KAZI KUU TANO (5) ZA IMANI KATIKA MAOMBI.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Uhusiano ni upendo unaozaa ushirikiano na mawasiliano kati ya pande mbili tofauti.
Kama tuna upendo kwa MUNGU inatupasa sana kushirikiana na MUNGU na kuwasiliana na MUNGU Mara kwa Mara.
Mawasiliano hayo ni maombi . Lakini maombi tu hayawezi kuzaa matunda kama sio maombi ya imani.
Kama kuna mambo matano(5) muhimu katika maombi yako basi ni hivi: 
=Jina la YESU KRISTO(Yohana 14:14), 
=Damu ya YESU KRISTO(Ufunuo 12:11),
= Neno la MUNGU la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU(Zaburi 107:20), 
=Nguvu za ROHO MTAKATIFU(Luka 1:35a
=Na Kuomba kwa imani(Waebrania 11:6)
Kama imani ni kitu muhimu kiasi hicho, je imani ni nini?
Biblia inajibu ikisema ''Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.-Waebrania 11:1''
Imani ni kuwa na uhakika na mambo yajayo.
Imani katika maombi ni kuwa na uhakika na ulichokiomba kwa MUNGU kwamba utakipata.
Kwa sababu imani ni kitu muhimu sana katika maombi, basi tuangalie kwa sehemu kazi za imani katika maombi.

Kazi Tano(5) za imani katika maombi.

1. Inakuondolea hofu, Woga na mashaka ndani yako.
 Isaya 54:14 '' Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.''
Hofu haitakukaribia maana utakuwa na imani kubwa ya ushindi.  

2. Inakufanya umwamini MUNGU.
Waebrania 11:8-11 ''
 Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni MUNGU. Kwa imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu.''
Biblia inaanza kwa kusema ''kwa imani'' maana yake imani ilifanya kazi kubwa sana hata wakafanikiwa hawa katika mahitaji yao, imani yao iliwafanya wamwamini MUNGU.
Kazi mojawapo ya imani ni kukufanya umwamwini MUNGU.
  
3. Inakupa kushinda
Mathayo 9:22 ''
 YESU akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.''
Imani ya Mwanamke huyu ilikuwa inaamini uponyaji wa Bwana YESU na hakika akapona saa ile ile.
Hata wewe kama unamwendea YESU kwa maombi ili akuponye au akutendee muujiza hakika imani yako inaweza kukupa kushinda kama kweli una imani kubwa ya kupokea ushindi kutoka kwa Bwana YESU.
Imani humpa  muombaji kushinda

4. Inakupa kuwa mwenye haki.
Habakuki 2:4 ''
Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.''
Imani yako kwa Bwana YESU imekufanya umwamini na kumpokea na hivyo kufanyika mwenye haki, kuwa mwenye haki ni kibali cha kupokea pia ushindi kupitia maombi. Imani katika YESU KRISTO inakufanya uwe mwenye haki.


5. Imani inakupa Ulinzi.
1 Petro 1:5 ''
 Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho. ''
Tunalindwa na nguvu za MUNGU kwa imani, hivyo imani inakupa ulinzi wa MUNGU maana unamwamini katika KRISTO.
Labda ngoja niseme pia neno hili.
Katika Agano la kale Neno ''Imani'' Linapatikana katika maandiko mawili tu yaani Kumb 32:20 na Habakuki 2:4 lakini matukio ya kumwamini MUNGU ni mengi sana sana na hayo yanaonyesha Imani hata kama Hakuna Neno Imani.

Unatakiwa sana kuomba kwa imani lakini pia licha ya jambo hilo muhimu sana unatakiwa pia kutunza maisha yako ya ndani ili kwa njia hiyo umruhusu MUNGU kukutetea katika maisha yako ya nje.
Tunza utakatifu,Tunza utu wako wa ndani ulio mzuri,Tunza utauwa.
Tunza ucha MUNGU wako ,Kwa hayo hakika utamruhusu MUNGU kukutetea pindi unapomuomba akutetee.

Kumbuka pia kwamba  MUNGU ni mkamilifu, Kazi yake ni kamilifu, Ametuumba kwa ukamilifu.
Akianzisha kazi huwa anaikamilisha.

Kumb 32:4 "Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. MUNGU wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili."
MUNGU ni mwenye haki,Kazi zake ni kamilifu.
Ahadi zake ni ndio na kweli,Yeye ni mwaminifu na mkamilifu.

Ndugu yangu, kutokumwamini MUNGU ni dhambi na ni kosa kubwa sana.
Ndugu usikubali dhambi ya kutokumwamini MUNGU muumba wako ikawa na wewe.
Nakuomba mwamini na mtii yeye na neno lake Biblia.

Isaya 40:28-31 "Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye MUNGU wa milele, BWANA, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia."
Neno hilo naomba nikusaidie kumwamini MUNGU na kumtegemea.
Imani hiyo ya kumwamini MUNGU katika KRISTO YESU itakupa ushindi Mkuu sana.

 Neema ya MUNGU iko pamoja wenye Imani watakatifu.
MUNGU ampe kila mmoja wetu roho ya kutubu na kuacha uovu, aliyepotelewa na ufahamu, ufahamu wake mzuri umrudie sasa.

Kuomba maombi ya imani ni jambo la muhimu sana ila zingatia pia na utakatifu sana katika maisha yako ya wokovu na maombi. 
 Baraka yako ni ya kwako tu hivyo ing'ang'anie.

Ngoja nikushauri pia kuhusu malengo yako. 
Ukiweka malengo mazuri kwenye maisha yako hakikisha.

1. Unayaombea malengo hayo.

2. Unamhusisha ROHO MTAKATIFU akusaidie katika kutimiza malengo hayo.
Kumbuka bila MUNGU wewe huwezi lolote hata unalodhani unaliweza, ndivyo Biblia inasema.
Yohana 15:5 "Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote."


3. Tafuta kusudi la MUNGU na kibali cha MUNGU ili kutimia kwa malengo hayo.

4. Anza kufanyia kazi malengo hayo, huku ukimshirikisha MUNGU kwa kila hatua.

5. Unaweza kumtolea MUNGU sadaka ya shukrani au sadaka ya nadhiri ili msaada wa MUNGU uambatane na wewe katika kukamilika kwa malengo hayo. 
Kumbuka ndani ya sadaka sahihi kwa MUNGU kuna agano na MUNGU (Zaburi 50:5) hivyo kufanikiwa inakuwa rahisi maana MUNGU analiangalia agano lake kupitia sadaka yako.


6. Ishi maisha matakatifu ya Wokovu daima, ili dhambi isikupate na kukuzuia kufanikiwa katika malengo yako.

7. Hakikisha malengo yako yanampa MUNGU utukufu wote.

Maombi ya Leo kwa imani.

1. Amuru nguvu za Giza ziachie afya yako, uchumi wako, uzao wako , ndoa yako na kibali chako.
Simama na Matendo 16:18


2. Omba kwa MUNGU kwamba ukae salama chini ya ulinzi wake.
Omba ndoa yako ikae salama.
Omba kazi yako ikae salama.
Omba uchumi wako ukae salama na omba uzao wako ukae salama.
Simama na Mithali 18:10


3. Muite MUNGU akuokoe katika kila eneo la maisha yako.
Simama na Zaburi 18:3


4. Fungua malango yako ya baraka zako yaliyokuwa yamefungwa.
Simama na Isaya 60:11
Kumbuka maana ya lango au malango ni mlango mkubwa wa kuingia katika mji au uwanja.
Kuna baraka zingine ziko karibu sana kukufikia kutokana na maombi yako na uaminifu wako kwa MUNGU ila ukifungua lango la kiroho utapata baraka yako ambayo inawezekana huwa unaiona tu kwenye ndoto kwamba unaipokea.
Leo omba na utamuona Bwana YESU akikushindia.


 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu. Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.
EV.MCHOME 
0672870833

Share this:

Post a Comment

 
Copyright © Yote Yanawezekana Kwa Yesu. Designed by OddThemes