Headlines

Kumjua Mungu

HIVI,NINAWEZAJE KUMJUA MUNGU WA KWELI?

Na Mch.G.Madumla.

Bwana Yesu asifiwe…
Chini ya jua hili,yupo mungu wa uongo pia yupo Mungu wa ukweli. Maandiko matakatifu yanathibitisha hili;
Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea;ambao ndani yaomungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.” 2 Wakorintho 4:3-4
Mstari huu,umetupa ufahamu mkubwa ya kwamba kuna mungu wa dunia hii lakini pia kuna Mungu muumba vitu vyote,vinavyoonekana na visivyoonekana. Na kumbe kuna kundi kubwa la watu wanaopotea ambao kwa hao injili ya kweli imesitirika yaani injili ya kweli haipo kwao,watu hao wapo nchini ya mungu wa dunia hii/miungu ya duniani isiyokuwa ya kweli ndivyo biblia isemavyo.
Leo hii kumezuka elimu nyingi zidanganyazo zikiwapotosha watu waiache imani ya kweli na kugeukia huko. Wengi wamekuja kwa jina la Bwana na kumbe sio,wakilitaja jina la Bwana huku wakiongozwa na miungu kwa siri kubwa sana,kwa maana hata hili si geni katika masikio ya watu wengi leo hii. Lakini vyema siku ya leo tukajifunza namna ya kumjua Mungu wa kweli.
Mungu wa kweli ni yupi?
Mungu wa kweli ndie Mungu aliyeziumba mbingu na nchi ( Mwanzo 1:1) na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Ni Mungu mwenye uweza,mamlaka na utiisho wa kipekee,ni Yeye aliyewaokoa wana wa Israeli utumwani Misri na ndie ametuokoa leo kupitia Kristo Yesu,tulipomuamini na kumpokea naye amekuwa Bwana na mwokozi wetu.
Zifuatazo ni njia tatu muhimu zinazotufunulia Mungu wa kweli,nasi tunamjua kupitia njia hizi;
01. KWA IMANI KATIKA KUSIKIA HABARI ZAKE ZILIZO SAHIHI.
Chanzo cha imani ni kusikia neno la Kristo ( Warumi 10:17). Kitendo cha kusikia habari sahihi za Mungu ni kitendo cha kwanza kinachotupa uhakika wa Mungu tunaemtumikia. Neno linalohubiriwa linafunua ukuu wa Mungu katika Kristo Yesu,na ndilo linajenga imani zetu kuamini nguvu na uweza wake Mungu. Tujifunze kwa neno la Mungu linasemaje katika hili;
Katika kitabu cha Matendo 17:16-23,Paulo anaona mambo ya ajabu yakitendeka hasa Athene mji uliojaa sanamu wakiabudu mungu asiyejulikana. Watu wa athene walikuwa watu wa kutafakari sana mambo ya dini,lakini hawakujua wanachokiabudu. Paulo anaanza kuwaeleza jinsi alivyo Mungu wa kweli alivyo,ili waweze kumjua na waachane na ibada za sanamu na wamtumikie Mungu wa kweli.
Maelezo ya Paulo sawa sawa na Neno,likawajenga imani kwa njia ya kusikia hata wengi wakamjua Mungu wa kweli. Tusome japo kidogo;
“ Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu.”  Matendo 17:29
Neno hilo liliwajenga imani wale waliokuwa wakidhani ya kuwa Mungu anaweza kuwa mfano wa dhahabu,fedha au vitu fulani vya kuchongwa na mwanadamu. Wale wote waliokuwa wakifanya ibada kwa mungu wa kutengeneza walikuwa hawamjui Mungu wa kweli. Sasa ilibidi elimu ya neno la Mungu itolewe kwao. Na kwa elimu hiyo,ikawapa imani kwa kuwa walisikia na kuelewa nayo.
Ndivyo ilivyo hata sasa;wapo watu wenye kujitengenezea miungu yao na kuiabudu wakidhani wanamuabudu Mungu wa kweli kumbe wanaiabudu miungu pasipo kujua kwa sababu mungu/shetani wa dunia hii amewapofusha macho ya mioyo yao wasione kweli wakaokoka. Kwa njia ya kusikia habari sahihi za Mungu wa kweli,tunamfahamu Mungu ijapokuwa kwa sehemu tu.
Leo,kuna mahali injili ya kweli haijafika. Hivyo watu hawana ufahamu sahihi kuhusu Mungu,kwa sababu tu hakuna wakuwahubiria na kuwafundisha habari za Mungu. Watu wa namna hiyo wanajiendea endea tu. Hata wewe singelikuwa kuhubiriwa habari sahihi za Yesu,ungemjuaje Mungu. Tujifunze kwa mtu wa Kushi,towashi aliyekuwa na mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi.
Mtu huyu alikuwa akiabudu asichokijua kwa muda wa miaka mingi. Akisoma habari za Yesu pasipo kujua kwa usahihi tena na kwa muda mrefu,hivyo ni sawa na kusema alikuwa hamjui Mungu wa kweli ingawa alikuwa na kiu naye kumjua. Towashi akakutana na Filipo alipokuwa akirejea kuabudu ameketi garini mwake na anasoma chuo cha nabii Isaya pasipo kujua kile akisomacho.
“ Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.” Matendo 8:31 ( Soma habari yote kuanzia 8:27 mpaka 39)
Angalia vizuri hapo,Towashi alipohubiriwa na Filipo habari za Yesu,gafura akafunuliwa na kuelewa sasa. Akabatizwa na kuokoka; lakini alikuwa hajui habari za Mungu mpaka alipojengwa imani yake kwa njia ya neno ndiposa akafahamu ni Mungu wa namna gani anayestahili kumfuata. Hata wewe unapaswa kusikia habari sahihi za Yesu,injili sahihi ya Yesu kusudi upate kujengwa kwake na kumjua Mungu wa kweli japo kwa sehemu.
02.MUNGU KUJIDHIHILISHA KWAKO.
Mungu anaweza kujidhihilisha kwako katika njia ya uponyaji kusudi umjue vizuri kwamba Yeye ni Mungu asiyeshindwa kitu. Lengo kubwa katika njia ni kukufundisha Yeye yukoje na anaweza kufanya yote katika yote ndio maana anakuponya. Tujifunze kwa mtu huyu;
Mtu mmoja aliyekuwa mwenye imani nyingine,alikuwa akitafuta uponyaji juu ya mateso yaliyokuwa yakimpata mara kwa mara. Mtu huyo alikuwa ni msomi mchumi fulani hivi kimasomo. Lakini majini na mapepo yalimsumbua sana,akajaribu hospitali lakini hakukua na majibu ya kweli. Akaenda kwa waganga akitaraji kupona lakini hawakufanikiwa. Naye alikuwa ni mkristo wa dini akiamini dini yake ndio sahihi bila wokovu.
Hivyo alipokuwa ameteseka kwa muda mrefu na kuchanganyikiwa. Siku moja alisikia mkutano wa injili,tena haukuwa ni mkutano mkubwa sana kiasi cha watu kusimama. Akajongea mkutanoni kusikiliza mahubiri maana kila mahali amejaribu na amekosa msaada. Anashuhudia mwenyewe kwa kusema ;
“ …nilimsikia muhubiri akisema,kuna watu wametembea kwa waganga wameteseka bila majibu,lakini leo kuna majibu ya kweli mahali hapa,akawa ananihubiria mimi yale yote…gafla nilijikuta nipo mbele,mhubiri akaanza kuniombea,na hapo yakanitoka mapepo,na huo ndio ulikuwa mwanzo wa kuokoka kwangu,tangu siku ile nilimjua Mungu wa kweli yukoje na mungu wa uongo yukoje...”
Wengi wamemfahamu Mungu kwa kuwa aliwaponya magonjwa yao,na kuanzia hapo wakapenda kusikia habari zake. Mimi ninaikubali sana njia hii ya kumjua Mungu,kwa maana nimeiona ikifanyika msaada wa kweli kwa watu wengi ninaowafahamu.
03. KWA KUFUNULIWA/ KUMUONA AKISEMA AU KUTENDA
Njia hii inaweza kumuelezea jinsi Mungu alivyo katika maono au ndoto ingawa si kwa watu wote. Kuna wakati Mungu anasema katika maono juu ya Yeye alivyo ili upate kumjua. Petro kuna kipindi alifundishwa na Mungu jinsi alivyo. Mungu alimfundisha somo kwamba Yeye Mungu hana upendeleo,sasa Mungu alitumia njia hii ya maono kusema naye;
Mungu anasema na Petro katika maono akimtuma kwa Kornelio. Kitu anachomuonesha ni cha ajabu kwake ( Matendo 10:9-16). Petro anapewa ufahamu kuhusu Mungu kwamba hana upendeleo,anamtuma hata kwa mataifa ambao walikuwa hawachangamani. Neno linasema;
`` Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;” Matendo 10:34
Nafasi ya Petro kujua hili,lilihitaji maono kwake. Tujifunze tena kwa Sauli aliyekuwa Paulo hapo baadae. Sauli aikuwa ni mshika dini,farisayo kweli kweli lakini asiyemjua Mungu wa kweli maana alikuwa bado chini ya sheria. Mtu huyu alimuudhi Mungu,kwa kuwaua watu wote wenye imani ya Mungu wa kweli. Hivyo,Yesu anamtokea akimtambulisha jinsi Yeye alivyo. Hii ikawa ndio njia yake ya kwanza ya Sauli kumjua Mungu wa kweli.
“ Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.” Matendo 9:4-5
Hatimaye,Sauli akawa Paulo. Yesu akajifunua na kusema naye,akamwambia kipi cha kufanya na kipi asifanye.  Hata leo Yesu U hai bado anatumia njia hii akisema nasi katika mafunuo kusudi tupate kumjua Yeye zaidi. Tunalion hili mara nyingi hata wakati wa maombi ya mifungo,wengine hupata maono na kusikia kile Mungu anataka kifanyike,na kupitia hicho tunaanza kumjua Yeye japo kwa sehemu.

Hivyo,njia tatu tulizojifunza leo kwa ufupi ni njia muhimu sana,lakini Mungu wetu hana mipaka anaweza kutenda yoyote ili wewe umjue vizuri
Ev.Mchome
0672870833

Share this:

Post a Comment

 
Copyright © Yote Yanawezekana Kwa Yesu. Designed by OddThemes