Headlines

Kwanini Israel

KWA NINI TUNAJIFUNZA KUHUSU TAIFA LA ISRAELI?

KWANI ISRAELI INATUHUSU NINI SISI?

EV.MCHOME  0672870833

Kwa vile tumeulizwa swali hili mara nyingi, ni vyema sana tukalijibu.

Wako waliotuuliza kwa ukali, kwa kejeli na wengine kwa ustaarabu, lakini ni jukumu letu kuendelea kuwa wapole na kumjibu kila mtu kwa upendo.

Awali ya yote tuseme yafuatayo:

Kwanza, tunasikitika kuwa WATU WENGI, TENA WAKRISTO, HUDHANI MUNGU HAJIHUSISHI TENA NA ISRAELI KAMA TUNAVYOONA AKIJIHUSISHA NAYO KWENYE BIBLIA!

Wanaona kama Mungu sasa amewaacha Israeli, na ni kama vile Mungu hana ishu tena na Israeli siku hizi.

Wanadhani Mungu hana kazi tena na Israeli leo!

Pili, hatukutegemea kuulizwa hili swali na mtu ambaye ni Mkristo.

Kwa nini?

Mkristo ni mtu anayetumia kitabu kiitwacho Biblia katika maongozi yote ya kumwabudu Mungu wa kweli.

Kitabu hiki hakikutoka Marekani, au Tanzania, au taifa lingine lolote, isipokuwa kilitoka Israeli.

Katika Biblia, neno Israeli limetajwa zaidi ya mara 2,300 (elfu mbili na mia tatu).

Biblia au Mungu  ametumia neno "watu wangu" mara mia moja na tisini na tano (195), akimaanisha Waisraeli.

Mara 21 kwenye Biblia Mungu amesema "watu wangu Israeli."

Neno "Mungu wa Israeli" limetajwa kwenye Biblia mara mia mbili na tatu (203) na ni huyo huyo Mungu wa Israeli ndiye na sisi tunamwabudu maana ndiye Mungu wa kweli.

Mara 177 Biblia imesema "Mungu wenu" ikimaanisha Mungu wa Israeli.

Mara 63 Biblia imetumia maneno "Mungu wao" ikimaanisha Mungu wa Waisraeli.

Kama unachukia taifa la Israeli, tazama vizuri hizo takwimu tulizotoa, uone kama utawachukia watu Mungu aliojitambulisha nao kwa kiwango hicho.

Tuendelee:

Haya tu yalipaswa kukufanya uanze kujihoji mwenyewe kwamba Israeli inakuhusu nini mpaka itajwe hivyo.

Kama hukujihoji lakini ukaendelea kuisoma Biblia, huku unashangaa watu wanapojifunza kuhusu taifa hili la Mungu, basi inaonekana kuna jambo haliko sawa, na lazima itakuwa kuna kitu umedanganywa au umejidanganya, HASA KUFIKIRI UNAWEZA KUHUSIANA NA MUNGU BILA KUHUSIANA NA ISRAELI.

Biblia yote ina masimulizi ya watoto wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, ambao wanaitwa Waisraeli.

Tunaposoma Biblia, hatuisomi kama vile watu wa kwanza kupewa yaliyomo humo, bali sisi ni wa pili, tukijifunza kwa hao ambao walipewa haya tunayoyasoma kwenye Biblia.

KUNA MAMBO MENGI AMBAYO MUNGU ALIWAPA WAISRAELI TU, NA KAMWE SISI TUSIO WAISRAELI HAYATAKAA YATUHUSU.

Ukishika Biblia, ni kama mfano umeshika kitabu chenye historia nzima ya Tanzania, lakini sasa hiki ni kitabu kinachoelezea habari za Waisraeli.

Tukiacha hayo, nchi ya Israeli, pamoja na udogo wake, ni nchi inayotatwa sana dunia nzima katika vyombo vya habari, ndio maana Israeli ni nchi maarufu mno duniani.

Angalao kwa sababu hizi chache za nguvu, inashangaza au ni aibu kwa namna fulani, ukikuta Mkristo anahoji tena kwa ukali; kwamba taifa la Israeli linatuhusu nini?

Kwa hiyo, kama unajua unamwabudu Mungu aliye hai, Mungu wa kweli, yule aliyeumba Mbingu na nchi, aliyekuumba wewe, basi UJUE UNAMWABUDU MUNGU WA ISRAELI.

Mungu hajawahi kujiita Mungu wa Tanzania, au Mungu wa Kenya, au Mungu wa Marekani, au Mungu wa Ufaransa, au nchi yoyote, bali siku zote Mungu amejifunua kwa kujiita Mungu wa Israeli.

Kama tulivyosema, katika Biblia, Mungu amejiita Mungu wa Israeli mara mia mbili na tatu (203)!!

Hata leo, kama Yesu angekutokea, katika utambulisho wake angefanya tu vile vile anavyofanya kwa wengine, angejiita "Mungu wa Israeli."

Mungu huyu wa kweli, alijifunua kwa ulimwengu wote kupitia taifa la Israeli.

Ili Mungu ajulikane kwa dunia nzima, ilibidi achague nchi moja ambayo kupitia hiyo angejifunua kwa ulimwengu wote.

MUNGU HAKUAMUA TU KUJIFICHA MBINGUNI, KISHA AKAANDIKA KITABU CHA KUMHUSU KISHA AKAKIDONDOSHA HUKU DUNIANI, KISHA AKABAKI HUKO MAFICHONI MBINGUNI.
HATA HIVYO HICHO KITABU INGEKUWA VIGUMU SANA KUKIELEWA.

Mungu alitaka ashuke kabisa na kujifunua kwa watu ili kupitia hao, dunia nzima imjue.

Sasa, Mungu aliamua kujichagulia wana wa Ibrahim, Isaka na Yakobo, yaani taifa la Israeli.

Sasa ona tena jambo hili;

Siku ile ulipomwamini Yesu kama Mwokozi wako, ukatubu na kubatizwa, yaani ukaokoka, ulifanyika mtoto wa Ibrahimu, yaani Mwisraeli kwa jinsi ya rohoni, bila kujali taifa unalotokea nje ya taifa la Israeli.

Mtu yeyote, haijalishi taifa analotokea, mradi amemwamini Yesu, anaungana na Waisraeli wale tu waliomwamini Yesu, kisha wote wanafanyika kuwa wana wa Ibrahimu.

Wagalatia 3:28-29
Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.

Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.

Kwa hiyo, kama umeokoka, wewe ni Mwisraeli, mwana wa Ibrahimu, pamoja na Waisraeli wote waliookoka kama wewe.

Kwa lugha nyingine, watoto wa Mungu duniani wanaitwa Waisraeli.

Mungu unayemwabudu ni Mungu wa Israeli, unatumia Biblia yao kumjua Mungu wa kweli, na unapomwamini Yesu unaunganishwa kuwa kitu kimoja nao.

Agano kuu kati ya Mungu na mwanadamu limefungwa kwa Waisraeli, wala sio nchi yako, au kanisa lako, na katika Agano la Kale, sisi tupo nje kabisa.

Ashukuriwe Mungu, kupitia Yesu, tunapookoka tunaingizwa kwenye hilo Agano kupitia Agano Jipya.

Tunaweza kusema kwa vile Mungu aliwachagua Waisraeli wawe watakatifu kwake, na ardhi ya taifa hilo iwe ni nchi takatifu kwake, basi Israeli ni makao makuu ya Mungu duniani.

Ni mahali pa Mungu pa kufikia.

Kama Mungu wetu ni Mungu wa Israeli, Mwokozi wetu anatokea Israel, wokovu wetu unatokea Israel,(Yohana 4:22), Kitabu cha Waisreli ndio kimetuongoza kumpata na kumjua Mungu wa kweli, na ile kwamba tunafanyika Waisraeli rohoni baada ya kuokoka, basi tuna kila sababu ya kuwa karibu sana na taifa hili la Israeli.

Tunapaswa kulipenda taifa la Israeli na kulibariki, la sivyo  hatutabarikiwa.

Baraka zote za Mungu duniani zinatokea Israeli na kusambaa duniani.

Ona Mungu alivyomwambia Ibrahimu:

Mwanzo 12:3
nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.

Tukiangalia Israeli kisiasa tutaishia kuwachukia tu, na ole wetu tukifanya hivyo.

Nitumie ujumbe kwa whatsapp nikutumie makala iitwayo: KWA NINI UNALICHUKIA TAIFA LA ISRAELI?

Muda wote tunatakiwa kuwa upande wa Israeli, kuwabariki, kuwaombea, na kuwatakia amani na ushindi katika vita vyote walivyonavyo.

Hatufanyi hivyo kwa sababu Waisraeli ni watu wazuri au watu wema, bali ni kwa sababu Mungu amewafanya kuwa watu wake, na hata Yeye Mungu hasemi amewachagua kwa sababu wana chochote kinachowafanya wastahili hiyo nafasi ya kuwa taifa takatifu kwa Mungu duniani.

Kumbukumbu 7:7-8
BWANA hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote;

bali kwa sababu BWANA anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu BWANA akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri.

Ni muhimu sana sana kufuatilia taifa la Israeli na yanayoendelea humo.

Kwa nini?

Unabii karibu wote unaohusu nyakati za mwisho unazingatia kinachoendelea nchini Israeli.

Dalili za nyakati za mwisho na matukio yake, hasa ili kujua dalili za unyakuo zimekaribia sana, tunatazama mwenendo mzima wa kinachotokea nchini Israeli na kile kinachowapata Wayahudi wote waliotawanyika duniani kote.

Mathayo sura ya 24, ni sura maarufu kwa sababu Yesu alikuwa anaelezea kwa undani kuhusu dalili na matukio ya siku za mwisho, ili kujua kuja kwa Yesu duniani mara ya pili kumekaribia kiasi gani.

Katika sura hiyo, mstari wa 32, anatuagiza tufuatilie matukio yanayotokea nchini Israeli.

Mathayo 24:32
Basi kwa mtini(Israeli) jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu;

Taifa la Israeli lilizaliwa tena tarehe 14 May 1948, baada ya kufutika kwenye ramani ya dunia kwa zaidi ya miaka 1,800!!

Huu ulikuwa ni unabii mzito sana kutokea nyakati zetu, na ni alama kubwa sana ya Unyakuo kukaribia mno.

Tuwasiliane nikutumie makala iitwayo: BIBLIA ILITABIRI ISRAELI ITAPATA UHURU MWAKA 1948?

Zaidi ya Maandiko 70 kwenye Biblia yametabiri Israeli itazaliwa tena na kuwa taifa siku hizi za mwishoni kabisa, baada ya kufutwa na Warumi mwaka 135BK.

Miaka 70 baadaye, tangu Israeli ilipozaliwa tena, mwaka 2017, kwa kusaidiwa na Marekani, Israeli ilifanikiwa kuufanya Yerusalemu kuwa ndio mji wao mkuu, baada ya kuzuiliwa na Umoja wa Mataifa kwa siku nyingi.

Hii nayo ilitufungua macho sana, maana kilio cha Waisraeli cha miaka yote ni kujenga tena Hekalu la Yerusalemu lililobomolewa mwaka 70BK kama Yesu alivyokuwa ametabiri.(Mathayo 24:2)

Weka sana akilini mwako, kwamba ISRAELI NI KAMA SAA YETU YA MKONONI, ambayo kwayo tunafuatilia kujua timeline nzima Yesu aliyotupa, ili tuwe Wakristo wanaoelewa kile kinachoendelea Mbinguni na kinachoenda kutokea duniani.

Tumepewa pia kazi ya kuombea taifa la Israeli.

Isaya 62:6-7
Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya;

wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.

Kama ni hivyo, lazima uwe mfuatiliaji wa ratiba ya Mungu duniani ili kujua upo majira gani, ndipo uweze kuomba unachotakiwa kuomba.

Vinginevyo, ukisikia kuombea Israeli utafikiri umeambiwa uwaombee labda wana shida ya mahitaji ya nguo na chakula, hivyo utaomba vitu ambavyo utaishia kuwachekesha malaika.

Share this:

Post a Comment

 
Copyright © Yote Yanawezekana Kwa Yesu. Designed by OddThemes