SOMO:- NAWEZAJE KUISHINDA DHAMBI
YA
TAMAA YA MWILI (NGONO) ?
[ Darasa la wavulana na mabinti ]
➖➖➖➖➖➖➖➖➖➖
Mstari muhimu wa kukumbuka:-
WAGALATIA 5:16-17:-"Basi nasema, ENENDENI KWA ROHO, WALA HAMTAZITIMIZA KAMWE TAMAA ZA MWILI. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka."
〰〰〰〰〰〰〰〰〰〰
Maadamu bado tumeuvaa mwili huu, basi sio kwamba kutamani hakutakuwepo kabisa. Kunaweza kuwepo! Lakini neno limetupa siri ya kuzishinda hizo tamaa za mwili kwa kuenenda kwa Roho Mtakatifu.
Neno la Mungu limeatuambia hapo mtu anayeenenda kwa Roho hataweza ```"KAMWE"``` kuzitimiza tamaa za mwili wake. Kuenenda kwa Roho ni kuishi maisha ya kutawaliwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu. Iko siri ya ajabu, uwezo na nguvu ya kuishi ndani ya Roho Mtakatifu kikamilifu. Ukiishi ndani ya Roho Mtakatifu kikamilifu hutaweza kamwe kuzitimiza tamaa zako za mwili labda ukatae tu mwenyewe kuenenda kwa Roho, yaani umuasi huyo Roho aliye ndani yako [ISAYA 63:10; WAEFESO 4:30].
Mojawapo ya faida kubwa ya mtu kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu tena na tena na akakubali kuongozwa na Roho Mtakatifu, kumtii. Huyu Roho humzuia mtu asitende dhambi, na hata kama kutakuwa na mitego ya kuwangusha mtu dhambini, huyu Roho atamwonyesha huo mtego na kumpa mtu hekima, maarifa na nguvu/uwezo wa kuishinda hiyo mitego ya Ibilisi [ LUKA 24:49; MATENDO 1:8; ISAYA 11:2]. ```Hata kama kwa hila za shetani utawindwa kiasi gani uangushwe```. Kwa mazingira kama hayo kama mtu uliyeookoka uko vizuri sana na Roho Mtakatifu, utasikia kabisa Roho anakwambia au kukuonyesha kitu: ```"Hapana! Hapana! Usiende! Usiende! Huo ni mtego. Jiepushe na huyo kaka au huyo dada, usichukue hiyo pesa, Zawadi.......... N.k."``` kuonywa huko na Roho Mtakatifu kutaambatana na kukoseshwa amani moyoni juu ya mtu fulani au jambo fulani linaloendelea. Na ukiwa mwepesi wa kumwelewa Roho Mtakatifu na kumtii kamwe hutaangushwa dhambini. Biblia inasema WAEBRANIA 3:12-13:-" Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa UDANGANYIFU WA DHAMBI".
Dhambi huwa inakuja na sura ya udanganyifu ili kumkamata mtu. Kwa nje inaoonekana nzuri, tamu, inapendeza lakini ndani imejaa sumu kali ya kukuua. Ni kama mtego wa ndoano katika kumkamata samaki. Ndivyo ulivyo ```UDANGANYIFU WA DHAMBI```, naam, dhambi ya zinaa. Inapokuotea ! [MWANZO 4:7]
Na ukiona hilo jambo unaloonywa na Roho Mtakatifu kibinadamu linakushinda nguvu moyoni. "Ni kama umishaanza kuvutwa kimapenzi na huyo mkaka au huyo mdada alivyo mrembo. Ameumbika mithili ya malaika! Duhu! Moyo umeshindwa kujizuia jamani, uko hoi! Wowowo! Tayari umefall in love". Lakini unasikia kuna kuonywa na Roho Mtakatifu ndani yako kuhusu hayo. Unachopaswa kufanya ni kutenga muda wa kufunga na kuomba kwa siku kadhaa, kwanza ukiomba TOBA kwa kumpenda. Na pili ukimwomba Roho Mtakatifu mwenyewe akuwezeshe na kukuongezea nguvu za kutoka katika hali hiyo. Jieleze wazi ulivyo dhaifu kwake, umedata. Mwombe Roho Mtakatifu nipeee nguvu, sitaki hali hii kabisa [WAEBRANIA 4:16; AYUBU 26:2; WAKOLOSAI 1:10-11].
Nakwambia ukimwendea Mungu kwa maombi ya uchungu na mzigo namna hii, BWANA YESU nataka kuishi maisha ya kukupendeza wewe lakini mwili unanishinda mimi. Roho Mtakatifu nisaidieeee! Endelea kulia na kulalama mbele za BWANA namna hiyo. Baada ya maombi ya namna hiyo ya kumainisha, ```UTAPOKEA UWEZO WA AJABU wa kuishi bila kumtamani mwanamke yoyote kiuasherati``` mpaka wakati wa ndoa. Wakati wengine dhambi ya ngono inawatesa na kuwatumikisha, kwako wewe utaikanyaga kanyaga dhambi hiyo chini ya miguu yako.
NAWEZAJE KUISHINDA DHAMBI YA TAMAA YA MWILI (NGONO)?
Biblia inasema enendeni kwa Roho wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili [ WAGALATIA 5:16-17].
Ili uishinde dhambi ya tamaa za mwili. Zingatia mambo yafuatayo:-
```(1) UWE UMEZALIWA MARA YA PILI KWA ROHO, yaani umeokoka.```
Kuokoka sio kubadili dini bali ni kubadilishwa maisha toka dhambini~gizani na kuishi katika nuru ya mapenzi ya Mungu. Lazima kuokoka kweli kuambatane na BADILIKO HALISI ndani ya maisha ya mtu [2WAKORINTHO 5:17].
Kuokoka kunaamhatana na mtu kupewa uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu, UWEZO huo ndio unaoitwa uwezo wa kushinda dhambi na kuishi kwa kumfanana Kristo Yesu ndani yako. Mtoto wa Mungu ni yule anayefanana na Mungu aliye na sura na mfano wake [ YOHANA 1:12-13; 1YOHANA 3:1-3; WARUMI 8:8-10].
Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani. Alikuwa ni mwanadamu kama sisi. Alibalehe kama tunavyobalehe sisi, alipevuka kama tunavyopevuka sisi. Lakini pamoja na hayo yote bado Yesu hakuwahi kumtamani mwanamke yoyote kiuasherati. Alijaribiwa sawasawa na sisi katika MAMBO YOTE bila kufanya dhambi [WAEBRANIA 4:14-15]. Na awaye yote ambaye amezaliwa mara ya pili na kuwa mtoto wa Mungu, anapewa uwezo wa kuwa kama Yesu. Tamaa ya uasherati haiwezi ikamsumbua sumbua, kiu ya ngono inazimishwa [WAGALATIA 5:24].
Na hata baada ya kuokoka. Hupaswi kuishia hapo tu. Lazima uendelee kuzingatia mambo mengine yafuatayo:-
```(2) EPUKA UKARIBU USIO NA MIPAKA KATI YAKO NA WAVULANA AU WASICHANA.```
Ukaribu uliopitiliza usio na mipaka uliopo kati yako na wavulana au wasichana, mwisho wa siku lazima utajikuta umeangukia kwenye dhambi ya uzinzi na uasherati tu. Huwezi kwepa!
Wengi waliosimama vizuri kiroho wameanguka katika dhambi ya zinaa, kwa sababu mojawapo ya kukosa ```nidhamu ya mipaka``` ya ukaribu wao na wasichana au wavulana (mazoea yaliyopitiliza ). Utaangushwa tu! Lazima mvulana ujitenge mbali na wasichana na msichana ujitenge mbali na wavulana [ MITHALI 6:23-29,32-33]. Simainishi kwamha msiongee au msishirikiane kabisa, la! Ila jiwekee ```NIDHAMU YA MIPAKA```, ukaribu uliopitiliza na usiokuwa na ulazima, na mazoea mazoea yasiyo na msingi. Block!
```(3) UNAPENDA KUSOMA NINI, KUSIKIA NINI NA KUONA NINI?```
Ukiwa kama kijana au hata mzee. Roho ya zinaa inapata mpenyo wa kumuingia mtu kupitia mambo makuu matatu ambayo ni:- ```Kusoma, kusikia na kuona```. Je unapendelea kusoma nini? Kusikia nini na kuona nini? Kama ni habari tu za mapenzi na ngono ndio unazijaza tu akilini mwako na moyoni mwako. Unapendelea kutazama video/tamthilia/ za mapenzi, picha za uchi, kusoma habari (magazeti) ya mapenzi ( mambo ya Sex sex tu). Hata kama umeokoka na unanena kwa lugha Lazima ROHO YA ZINAA itakuingia tu na utaangushwa mweleka.
Ili uishinde tamaa ya mwili (ngono) . Lazima pia ujitawale au ujizuie na kule kusoma kwako, kusikia kwako na kuona kwako. Wekeza sana zaidi kupenda kusoma neno la Mungu, kusikia nyimbo/mahubiri ya neno la Mungu na sio miziki hii ya kidunia, na kuona yale yaliyo mema yanakusogeza karibu zaidi na Mungu iwe kwenye picha/video au Internet na sio yale ya kidunia yanayokuingizia roho nyingine ya tamaa ndani yako. EPUKA, YAKIMBIE! [ ZABURI 101:3; WAKOLOSAI 3:16; ZABURI 119:11].
```(4) UWE NA MAISHA YA KUFUNGA NA KUOMBA KWA MUDA MREFU!```
Kamwe huwezi kuishinda nguvu ya tamaa ya mwili, kama huna maisha ya kufunga na kuomba kwa muda mrefu. Tunakumbuka Yesu alisema ombeni msiingie majaribuni, roho i radhi lakini mwili ni dhaifu [ MATHAYO 26:40-41]. MAOMBI YA KUFUNGA ya mara kwa mara na ya muda mrefu yanaudhoofisha na kuufunga mwili na kuipa NGUVU ROHO YAKO kuutawala mwili. Hivyo tamaa nyingi za mwili kwa mtu ambaye ni ```mwombaji sana mzamiaji```, tamaa za mwili kwake huwa hazimsumbui wala kumchukua tofauti na mtu ambaye sio ```mwombaji mzamiaji```. Maombi ya muda mrefu hasa ya kufunga yanakata kiu ya dhambi ndani ya mtu na kumpa nguvu za kiroho za kutembea katika usafi na utakatifu.
```(5) JIHADHARI NA KUJIEPUSHA NA MARAFIKI WASIOMJUA MUNGU.```
Ukitaka kuishinda dhambi ya tamaa ya mwili lazima pia ujidhari na marafiki ulionao. Biblia inasema tembea na wenye hekima na utakuwa na hekima bali Rafiki wa wapumbavu ataumia. Tena marafiki wabaya huharibu tabia njema [MITHALI 13:20; 1WAKORINTHO 15:33 Kjv].
Ukiishi na kutembea na company ya marafiki wazinzi, wapenda ngono na anasa za dunia hii. Hawawazi juu ya Mungu hata kidogo bali wao wanawaza juu ya mambo ya kidunia tu. Hata kama umeokoka, usipojiepusha nao, watakuambukiza hiyo tabia yao na taratibu kidogo kidogo utaanza kuvutwa na kuwa kama wao, utafanana nao. Upende au usipende watainyonya nguvu yako yote ya kiroho na kukumaliza [ HOSEA 7:8-9].
Ukiwa chuoni, shuleni, nyumbani na popote pale jitenge na company ya marafiki wasio na hofu ya Mungu ndani yao. Nitajuaje kama hawana hofu ya Mungu? Jibu:- Angalia wanaogopa kutenda dhambi hata iliyo ndogo. Kama ndani yao HAWAOGOPI KUTENDA DHAMBI. Basi jua kwamba hawa ni marafiki wasio na hofu ya Mungu. Jiepushe nao! [ ZABURI 1:1-3; ZABURI 26:2-6; MITHALI 1:10, 15-16; 22:24-25]. Bali unapaswa kukaa na kuzungukwa na marafiki waliojaa hofu ya Mungu ndani yao ambao wanazingatia kuishi katika usafi na utakatifu wa Mungu ndani yao katika usemi, tabia na mwenendo wao wote [ MITHALI 16:6,17; 2TIMOTHEO 2 :19-22; 1PETRO 1:15-16].
Ni bora kuishi bila marafiki kabisa kuliko kuwa na marafiki wanaokupekeka na kukuvuta Jehanamu ya moto kila siku.
```(6) ACHA MAVAZI YA MITEGO BALI VAA MAVAZI YA KUJISITIRI (KUJIHESHIMU).```
Huwezi kuwa wewe ni binti na umeokoka ukaishinda dhambi ya tamaa ya mwili kama huwa makini na jinsi yako unavyovaa . Unawavalia wanaume mavazi ya mitego halafu unakemea pepo la ukahaba lisikufuatilie. Wapi na wapi? Unatwanga maji kwenye kinu mpendwa. Ni sawa na mtu aliyetapakaa kinyesi mwili wote akijaribu kuwafukuza nzi wasimfukizie badala ya kujisafisha kwanza. Hao nzi hawatakuacha, watakufuata tu!
Ndivyo ilivyo mtu anayekemea pepo kahaba lisimfuate fuate huku hataki kuacha kuvaa mavazi ya kikahaba ya kuwatega wanaume! Kemea ujuavyo Mapepo ya ukahaba hayawezi kukuacha mwanamke!
Biblia inasema katika YEREMIA 31:22:-" Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; MWANAMKE ATAMLINDA MWANAUME"
Ni wajibu wa wanawake wanaomjua Mungu kuwalinda wanaume. Acheni kuvaa mavazi ya mitego! Epuka kuvaa suruali, vimini, vipedo, skenitaiti, mavazi ya kubana mwili na kuachia maungo yako wazi:- matiti, mapaja, kitovu na ```mapambo ya kidunia```:- mahereni, bangili mikufu, kutinda nyusi, wanja, lipostiki, rasta, mawigi na makorokoro yote ya urembo n.k. Nyuma ya mapambo yote hayo ya kiduniani kwa wanawake yameambatana na ```roho ya ukahaba na uchawi```. Ndiomaana unajiwa na ndoto za kufanya mapenzi usiku pengine na watu hata usiowajua [ MITHALI 7:10; KUMBUKUMBU 22:5; YEREMIA 4:30; 2WAFALME 9:22,30; ISAYA 3:16-24; 1PETRO 3:2-6]].
Kama wewe ni binti uliyeokoka acha kujipamba kidunia, zingatia kuvaa mavazi mazuri ya kujisitiri, ya kujiheshimu mbele za Mungu na hata mbele za wanadamu siku zote [ 1 TIMOTHEO 2:9-10].
```(7) USIJIINGIZE KATIKA MAHUSIANO YA KIMAPENZI KABLA YA WAKATI WA KUOA AU KUOLEWA```.
Biblia inatuonya juu ya jambo hilo ikisema katika
WIMBO ULIO BORA 2:7"-"Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe."
Kila jambo lina wakati wake. Ni makosa kuthubutu kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi kabla ya wakati wako maalumu wa kutaka kuoa au kuolewa.
Kama wewe ni mwanafunzi, au uko chuoni au bado kwanza unatafuta zako maisha, hujafikia kipindi cha wakati wa kuamua sasa kutaka kuoa au kuolewa. Usithubutu kutaka kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na mtu yoyote. Vinginevyo utaanguka tu dhambini.
Kama katika mipangilio yako ya kimaisha hujafikia bado kipindi cha wakati wa kufanya maamuzi ya kutaka ```SASA``` nioe au kuolewa. Usianzishe mahusiano ya kimapenzi na mtu kwa kisingizio cha kwamba TUTAKUJA KUOANA BAADAYE. Mnajidanganya ninyi shetani atakuja kuwajaribu na mtaanguka dhambini bila shaka. Na mnaweza msije hata kuoana.
Kipindi cha kuwa na mchumba lazima kiwe ndani ya wakati wako muafaka wa kutaka kuoa au kuolewa. Usije ukaweka mahusiano na mkaka au mdada fulani ambaye hajafikiria kuolewa leo wala kesho! Mwisho wa siku katika safari ndefu ya mahusiano yenu mtaanguka katika dhambi ya tamaa ya uasherati.
Hivyo basi ni afadhali usiyanuse wala kujihusisha na mapenzi kabisa mpaka pale utapofikia wakati wako wa kutaka kuoa au kuolewa! Ndipo ufikirie kuwa na mahusiano. Nje na hapo, usithubutu!
Hiyo ndiyo siri ya ushindi kwa kijana anayetaka kuishinda dhambi ya tamaa ya mwili. Zingatia hayo mambo saba kikamilifu, kaa katika hayo na yaishi hayo. UTASHINDA!
1 YOHANA 5:4:-"Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu."
Hili ndilo jibu langu kwa mabinti na vijana wanaoniuliza.
🌸🌸🌸🌸🌸🌸🌸🌸🌸🌸
Ukipenda kuwasiliana nami kwa ushauri , maombezi na mafundisho zaidi ya masomo ya neno la Mungu. Karibu :-
0672870833
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment