*Unafanyaje wakati wa Anguko la Kimaisha?*
*EV.MCHOME *
Maisha ni shida na raha, kupanda na kushuka. Hata hivyo, uwezo wa kuhimili na kuzishinda changamoto na maanguko ya kimaisha hutofautiana baina ya mtu mmoja na mwingine.
Baadhi yetu tukifikwa na misukosuko na maanguko ya kimaisha, hujikokota, hunyanyuka na kupanda tena, lakini wengine mabalaa ya kimaisha hutumaliza kabisa. Hutufanya tuanguke moja kwa moja. Hutufanya tupotee kabisa kutoka katika hadhi na aina ya maisha bora tuliyokuwa tunaishi.
Ni kwa namna gani unaweza kukabiliana na shida , balaa au mgogoro pale maisha yanapokuwa yamekupiga kiasi kwamba unaona huwezi kusimama tena?
Unafanyaje pale kila kitu kinakwenda kinyume nawe? Unapoteza kazi, nyumba na gari...pale unapopoteza uwezo wa kufikiri kwa usahihi?
Unafanyaje pale kampuni haikuhitaji tena?Unafanyaje unapokuwa umepoteza kipato?
Unafanyaje pale hata marafiki hawawezi kukusaidia na badala yake wanafunga milango?
Unafanyaje pale mfumo tegemeo wa maisha yako unapokuwa umekutupa nje?
Unafanyaje pale kampuni inapofilisika au unapoteza kazi?
Unafanyaje pale wadeni wako wanapokusukuma ukutani wakitaka uwalipe? Unawezaje kupita katika hali ya namna hiyo?
Embu piga picha umefanya kazi kwa miaka 30 sasa, lakini kazini kwako hawakutaki tena na umezeeka huwezi kujifunza ujuzi mpya, unafanyaje?
Unafanyeje pale kampuni ya Bima inapokuwa haitaki tena kukudhamini kwa kuwa inaona huna faida kwa kuwa ni mzee? Na kwa sasa huendani na sera wala kanuni zao!
Unafanyaje pale magonjwa yanapokuzidia na kuzidiwa na gharama za matibabu, pesa zote zinakwenda kwenye matibabu na unauza kila kitu ulichokuwa nacho?
Unafanyaje pale msongo wa mawazo kwa kukosa kazi na pesa unasababisha hata msielewane na mwenzi wako? Unafanyaje?
Lazima ufanye kitu. Lazima ujinasue. Kutohimili na kulishinda balaa la kimaisha, kutaruhusu kifo kibaya cha maisha duni, ya mateso na fedheha ya kudumu.
Ni katika shida hiyo hiyo au balaa hilo hilo ndipo ilipo siri, akili, nguvu na morali ya kukuwezesha sio tu kujikwamua bali kufanikiwa upya kimaisha, tena pengine mara nyingi kuzidi yale mafanikio uliyokuwa nayo kabla ya kuanguka.
Shida au balaa la maisha linakupa fursa zifuatazo:
Kwanza, shida inakulazimisha namna mpya ya kufikiri. Fikra huwa hazina mwisho. Baadhi yetu hubweteka. Tunapokuwa katika maisha mazuri...huwa hatushughuliki tena na ulimwengu wa kufikiri. Shida hutufanya tufikiri kwa kina na kwa kasi zaidi na kupitia fikra shida hutuonyesha fursa na namna mbadala za kujikwamua kimaisha ambazo tusingeweza kuziona hapo kabla.
Ni pale unapopitia changamoto, ndipo akili inaanza kupekua, kuangalia,na kutafuta suluhishio. Albert esteen anasema, kamwe hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kipimo cha akili ile ile iliyo leta matattizo haya. Changamoto hupelekea akili zetu kupevuka. Inasemekana akili huwa inakuwa na makali sana yaani (sharp) pale mtu anapokuwa na shida .
Pili, shida inakutoa kwenye maisha ya mazoea. Baadhi yetu huanguka moja kwa moja kwasababu ya kutokukubali (spirit of denial) kuwa tumefikwa na balaa kubwa na lazima kutafuta namna mbadala ya kujikwamua. Ni lazima ukubali kuwa huwezi tena kuishi kwa kutegemea kazi ile ile uliyokwishaipoteza...au kwa kuutegemea ujana ule ule uliokuwa nao wakati umeshazeeka. Hatua muhimu sana ya kujikwamua ni kukubali kuwa ni lazima ubadilike.
Shida hufuta mazoea. Mazoea ni mabaya. Mazoea yanatufanya tubweteke. Mazoea yanatuzuia kukua. Mazoea ni hatari. Tunapopitia shida, tunajikuta ni ngumu kuendelea kufanya jambo tulilozoea kutokana na mazingira kutokuruhusu tena. Na ni pale tunapoachana na mazoea, ndipo akili yetu inaamka!
Tatu, kama wewe ni kiongozi shida huonyesha na kudhihirisha uwezo wako wa uongozi.
Shida huibua na kuthibitisha uwezo wa kiongozi. John Maxwell anaeleza wazi; hakuna kitu kinampa kuaminika kiongozi kama uwezo wake wa kukabiliana na changamoto (It gives credibility) Changamoto zinapoibuka, ni kiongozi mwenye uwezo wa kuzikabili na kuzitatua na hivyo humpelekea mtu huyu kujitambua/ kutambulika kuwa yeye ni kiongozi na hatimaye, kuimarika zaidi kama kiongozi.
Viongozi huaminiwa zaidi wanapojaribiwa katika shida na kushinda . Kama kiongozi unaaminiwa unapokuwa tested.
Nne, Shida zinadai ubunifu. Changamoto inapokubana, mara nyingi namna pekee ya kuchomoka ni kuwa mbunifu. Kubuni kitu cha utofauti, aidha wazo la biashara, au namna tofauti ya kuwasilisha hoja yako au namna mpya ya kutengeneza kitu fulani. Unapokuwa mbunifu katika shida, unakuwa na nafasi nzuri ya kuikabili shida kwa ujasiri.
Tano, Shida hupelekea kukua na huleta maendeleo. Hakuna shida, hakuna maendeleo. Bwana Theodore Rubin anasema, tatizo sio kwamba kuna matatizo, tatizo ni kutegemea tofauti na kufikiri kuwa na matattizo ni tatizo. Ni mhimu kuanza na fikra hii; Matatizo si tatizo, ni sehemu tu ya maisha, ukiwaza hivi, akili yako ina Kuwa. Kwani untaanza kutazama zaidi namna ya kuwa bora. Usitamani iwe rahisi, tamani uwe bora zaidi , ili uwe na uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazokukabilii.
Kwa kumalizia, ubunifu wa madawa ulikuja baada ya Kuwa na shida ya magonjwa, magari, ndege, meli baiskeli, pikipiki vilibuniwa baada ya Kuwa na shida ya usafiri.
Katiba nzuri na bora ziliandikwa baada ya kupitia uongozi mbaya na katili.
Shida ilimfanya mwanadamu agundue moto.
Tumia shida , baa , janga au changamoto kukutoa hapo ulipo.
Mpaka wiki ijayo Mungu akitupa uzima , ningependa kusikia kutoka kwako , Tuma sms kunipa maoni yako kwa 0672870833
Kuhusu HOJA FIKIRISHI
Home > Wasaka mafanikio > Unafanyaje wakati wa anguko la maisha
Unafanyaje wakati wa anguko la maisha
By Yote Yanawezekana Kwa Yesu • December 23, 2019 • Wasaka mafanikio • Comments : 0
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment