Headlines

Maagano ya damu

MIKATABA (MAAGANO) YA DAMU
Kifungo au mkataba mkubwa kuliko yote ni kifungo/mkataba wa damu, kile kifungo/mkataba uliokufunga wewe ukaitwa mwana wa Mungu ni mkataba wa damu ya Yesu Kristo. Mungu ni Mungu wa mikataba ndio maana anaitwa Mungu ashikaye maagano yaani ukiingia naye mikataba huwa haivunjiki na kila alipokutana na mtu kwenye agano la kale hakuivunja. Mungu akifunga mkataba na wewe huwa hauvunji.
Mwanzo 6: 18 “Lakini nitafanya agano langu nawe kuwa thabiti; nawe utaingia katika safina, wewe, na wanao, na mkeo, na wake za wanao, pamoja nawe.”
Mwanzo 15: 18 “Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati”
Mungu alimuahidi Ibrahimu atamfanya naye mkataba wa kuitwa Baba wa watoto wengi japo alikuwa mzee sana. Wakati huo Ibrahimu alikuwa anajulikana kama myahudi, na kipindi kile kulikuwa hakuna agano la waisraeli lakini Mungu alifanya naye agano kwa kumpa nchi ya watu wakanaani, wayebusi nk.
Ezekieli 16:20 “Pamoja na hayo uliwatwaa wana wako na binti zako, ulionizalia, ukawatoa sadaka kwao ili waliwe. Je! Mambo yako ya kikahaba ni kitu kidogo tu”
Kuna wakati huna watoto, nyumba, huna chochote lakini Mungu akikuangalia anakuona unamiliki vitu vingi. Mungu alimtoa Ibrahimu kutoka kwenye nchi ya Baba yake na kufanya naye agano kipindi hicho kabla hajamzaa Isaka. Wakawa wanakaa kwenye nchi hiyohiyo akazaliawa Yakobo mpaka Yusufu na ndugu zake Yusufu wakamuuza akaenda kwenye nchi ya utumwa miaka mia nne na thelathini yeye na Yakobo na ndio maana Mungu alikuwa anawaambia wayahudi watakula na kukaa sehemu ambayo hawakuijenga sababu walipokuwa utumwani walikuja watu wengine wakakaa kwenye ile nchi ya ahadi wakajenga na kufuga na kulima.
Mungu alipomtokea Musa alijitambulisha yeye kama Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo akimaanisha bado anashikilia lile agano alilofunga na Ibrahimu kwamba wataimiliki nchi ya ahadi. Na hata wewe leo inawezekana upo kwenye utumwa usiogope sababu yupo Musa wako ambaye atakurudisha mahali alipokupa Bwana. Wanadamu wakikupa wanakunyang’anya muda wowote lakini ukipewa na Bwana vinadumu na hakunyang’anyi.
Mungu alisema atakayetokea yeyote kuzuia auwawe ndio maana maji yalipokosekana aliuambia mwamba toa maji, ndio maana wayebusi walipojaribu kuzuia aliamuru wachinjwe wote ili agano lake litimie. Mungu akitaka kukupa huwa hasubiri mpaka kiti kiwe wazi hapana, anakuambia wakati kiti kikiwa kinamilikiwa na mtu baadaye ndipo anayeshikilia anaondoka. Mungu akisema amekupa amekupa.
Njiani hapo kuna Wanefili, Waamaelki, Wayebusi, kuna bahari ya shamu hao wote ni wazuiaji lakini hawawezi kukuzuia wewe usimiliki. Ukitenda mambo mema Mungu anaangalia mpaka kizazi chako cha nne.
Leo tunavunja mkataba na kutengeneza mkataba mwingine. Ndio maana Mungu alimwambia Sulemani angemwangamiza lakini kwaajili ya Baba yake Daudi hatamwangamiza. Chagueni ni nani mtakayemtumikia lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.
Anayekuonea hana mkataba na Bwana wewe mpige kwa mapigo ya upanga. Wale waisraeli walishaambiwa na Mungu kwamba nchi ile alishapewa na Baba yao Ibrahimu hivyo wakimkuta. Kwenye nchi ile ya ahadi kulikuwa na wenyeji walioitwa wagibeoni ambao walisikia habari za waisraeli wamemchinja mfalme ogu kama mbuzi, wamewachinja waamori wote hivyo wakaamua kutaka kujiunga na wana wa Israeli lakini haiwezekani kuungana nao kama wanakaa ndani ya nchi ya Israeli.
Kulikuwa na wazee ambao waliamua kumfuata Joshua na kumwambia wametoka mbali zaidi ya nchi ile ya ahadi wanayoiendea wana wa Israeli na nguo zao zilikuwa zimechakaa na viatu vyao pia ndipo Joshua akawaapia kwa jina la Bwana hatawauwa na akawaandikia na mkataba. Sasa wana wa Israeli walipoingia kwenye nchi ya ahadi wakawakuta wale wagibeoni na wao wakajitetea wasiuwawe sababu wameshasaini mkataba nao.
Wana wa Israeli walipokaa kwenye nchi yao kwenye miaka 70 wakachukuliwa utumwani tena shushani ngomeni kwa mfalme wa Babeli lakini walikuwa pamoja wakaishika mila yao. lakini Mungu aliwarudisha.
Kwenye karne ya kwanza mwaka wa 70 wakasambazwa duniani kote na warumi (waroma) mpaka kwenye mwaka wa 1947 wakaanza kurudi mmoja mmoja kukusanyika na kumpiga mfilisti (Mpakistan) ndio maana leo waarabu wanalalamika wayahudi ni waonevu kwasababu wamekaa kwenye nchi hiyo tangu mwaka wa 70. Na kwa bahati mbaya sana wayahudi wanatumia torati yaani vile vitabu vitano vya Musa na wanaangalia wamepewa kutoka kwenye mto frati mpaka mahali fulani, wao hawaangalii sheria ya umoja wa mataifa. Na juzi juzi umoja wa mataifa umeamua kususia bidhaa zitokazo Israeli lakini wao wapo.
Mungu ni Mungu wa maagano, haijalishi nani anazuia akisema amekupa ameshakupa. Imekuwepo mikataba kati ya Mungu na wanadamu imekuwepo mikataba kati ya wanadamu na wanadamu na tunaangalia mikataba kati ya wanadamu na mashetani.
Isaya 28: 15 “Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli; kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka. Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo timazi; na mvua ya mawe itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri.”
1Samweli 23: 17 “Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa wa pili wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu. Na hao wawili wakafanya agano mbele za Bwana; Daudi naye akakaa huko Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani kwake.”
Yoshua 2: 1 “Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kutoka Shitimu kwa siri, ili kupeleleza, akawaambia, Enendeni mkaitazame nchi hii, na Yeriko. Wakaenda wakafika nyumbani kwa kahaba mmoja jina lake aliitwa Rahabu, wakalala huko. Mfalme wa Yeriko akaambiwa, kusema, Tazama, watu wawili wa wana wa Israeli wameingia humu leo usiku, ili kuipeleleza nchi. Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akasema, Watoe watu wale waliokuja kwako, walioingia ndani ya nyumba yako, maana wamekuja ili kuipeleleza nchi. Yule mwanamke akawatwaa wale watu wawili, akawaficha, akasema, Naam, wale watu walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka; ikawa kama wakati wa kufungwa lango la mji, kulipokuwa giza, watu wale wakatoka, wala sijui walikokwenda; wafuateni upesi, maana mtawapata. Lakini yeye alikuwa amewapandisha darini, akawaficha kwa mabua ya kitani, aliyokuwa ameyatandika juu ya dari. Basi hao watu wakawafuata kwa njia iendayo Yordani mpaka vivukoni; na mara wale watu waliowafuatia walipokwisha kutoka, wakalifunga lango. Tena kabla hawajalala akawaendea juu darini, akawaambia wale wanaume, Mimi najua ya kuwa Bwana amewapa ninyi nchi hii, na ya kuwa hofu imetuangukia mbele yenu, na ya kuwa wenyeji wote wa nchi wanayeyuka mbele yenu. Maana tumesikia jinsi Bwana alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu, hapo mlipotoka Misri, tena mambo hayo mliyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa huko ng’ambo ya Yordani, yaani, Sihoni na Ogu, mliowaangamiza kabisa. Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini. Basi sasa, nawasihi, niapieni kwa Bwana, kwa kuwa nimewatendea ihisani, ya kwamba ninyi nanyi mtaitendea ihisani nyumba ya baba yangu; tena nipeni alama ya uaminifu; ya kwamba mtawaponya hai baba yangu na mama yangu, na ndugu zangu wanaume na wanawake, na vitu vyote walivyo navyo, na kutuokoa roho zetu na kufa. Wale wanaume wakamwambia, Uhai wetu badala ya uhai wenu, ikiwa hamwitangazi habari ya shughuli yetu hii; kisha itakuwa, wakati Bwana atakapotupa nchi hii, tutakutendea kwa ihisani na uaminifu. Ndipo akawashusha kwa kamba dirishani, maana nyumba yake ilikuwa katika ukuta wa mji; naye alikaa ukutani.”
Mikataba na shetani inaweza kuwa ya kuwauwa watu kwaajili ya utajiri, mikataba hii ya utajiri wa haraka na kufa baada ya muda , yaani mtu awe tajiri kwa kutoa damu au kumtoa mwanaye awe sadaka ili kusudi afanikiwe.
2wafalme 3: 26 “Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.”
Wayahudi walikuwa wanaziona dalili zote za ushindi ziko zinaonekana lakini mfalme wa edomu akaamua kutumia silaha yake ya mwisho ndipo akamchukua mwanaye akamchoma na mkuki akamchinja akamchoma moto na wayahudi wakakimbizwa na mashetani wakashindwa. Unaona mikataba na mashetani kama hii inaweza kufanyika kwaajili ya kupata uongozi, kufanikiwa kibiashara, kufanikiwa kisanaa inafanyika.
Kuna wakati inaonyesha dalili utashinda lakini mwenzako anakimbilia mahali anakwenda kutoa kafara na wewe unakaa kimya huwezi kusema lolote. Kuanzia hapo mtu huyo aliyetoa kafara anakuwa mali ya shetani yeye na uzao wake ndio maana tunaivuja mikataba ya damu na kuweka mikataba ya Yesu.
MIKATABA YA MANENO.
Mikataba hii waganga wa kienyeji huifanya pale wanapochanja chale wateja wao hutamka maneno ambayo mashetani huyasikia na kuyashikilia kizazi mpaka kizazi.
Mithali 6: 2 “Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako.”
MIKATABA YA YA DAMU
Biblia inasema hakuna agano pasipo damu.
Mambo ya walawi 17: 11 “Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi.14 Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.”
Kumbe uhai wa mwili upo katika damu, kifungo kikubwa mtu akichukua damu amekuchukua wewe ndio maana Biblia inasema damu na nyama havitaurithi Ufalme wa Mungu. Mtu akichukua damu yako anaumiliki uhai wako na mifupa yako, amechukua misuli yako amechukua kila kitu kwasababu uhai umo katika hiyo damu. Kwasababu ndani ya damu kuna chembe hai ambazo zinatengeneza ogani mpaka wewe mwenyewe.
Ina maana unapoiacha damu kwa mganga wa kienyeji umejiacha wewe kwa mganga wa kienyeji uko kule na akili yako iko kule na moyo wako uko kule.
Ndio maana damu ya Yesu ni uhai wa Yesu na ilimwajika kwenye ardhi ambayo kila mtu ameumbwa kwayo. “Nao wanamshinda kwa damu ya Yesu”.
Wewe unaweza ukawa unahisi umelogwa leo kumbe ni ile damu ambayo wewe au baba yako aliiacha kwa mganga wa kienyeji anaitumia.
Unaweza kujisikia mwili unawaka moto jibu ni kule kwa mganga wa kienyeji wanasababisha. Mchawi akiipata damu yako amekupata wewe na kama hujaokoka ukiwaza kufanya jambo la maana huwezi sababu ya ile damu yako ipo kwa mganga. Unaweza ukawa huoni ghafla na ukienda hospitalini wanakupa miwani yenye lensi kubwa ajabu na wao wachawi wanafurahia sababu hujui ni wao wamesababisha.
Unaweza ukawa umeokoka lakini shida zinakufuata bado sababu rohoni uko huru lakini mwilini shetani anakuchezea sababu anaimiliki damu yako.
Mwanzo 9: 4 “Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile.”
Kumbukumbu la torati 12: 23 “Ila ujihadhari kwamba usile damu, kwani ile damu ndiyo uhai; na uhai usile pamoja na nyama. Usiile; imwage juu ya nchi kama maji. Usiile; ili upate kufanikiwa, na watoto wako baada yako utakapofanya yaliyoelekea machoni pa Bwana.”
Damu ni uhai na kitu kilicho na uhai kina tabia na inasauti na inaweza kutembea na mtu.
Mwanzo 4: 10 “Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.”
“Leo ninavunja mikataba ya damu kwa jina la Yesu”
Inaweza kuzungumza afe! Afe! Afe!, awe tasa! asisafiri, augue n.k. Damu inaposema afe ndio sasa mashetani wanakuja kukaa kwako, damu ikizungumza asiolewe!asiolewe! mashetani yanakuja kukaa kwenye sura yako unakuwa unatisha, damu inapozungumza talaka! Talaka! talaka mashetani yanakuja kwenye ndoa yako na kuvunja.
Yeremia 26: 15 “Lakini jueni yakini ya kuwa, mkiniua, mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia itakuwa juu yenu, na juu ya mji huu, na juu ya wenyeji wake; kwa maana ni kweli Bwana amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia.”
Ndio maana wakati Yesu anahukumiwa Pilato alinawa mikono akasema damu ya mtu huyu isiwe juu yangu na wayahudi wakasema iwe juu yao na watoto wao.
“kwa damu ya Yesu kuanzia Leo ninavunja mikataba ya Damu kwa jina la Yesu.
Watu wengi hawajui njia ya Yesu imejazwa na Damu tangu alipokuwa gethemane damu iliyomwajika ilikuwa inanena mema.
Waebrania 12: 5 “Tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye.”
Damu ya Yesu ina sauti ina maneno mazuri juu yetu.
Isaya 53: 5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Yesu alipigwa mijeledi mitatu kwa pamoja mara kumi na tatu na Isaya Imeandikwa kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
Damu nyigine ni ile iliyotoka miguuni ambao ni mkataba wa kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za kutoka kuzimu.
Huu ni mkataba wa Uponyaji tulionao. Damu nyingine ni ile ya mikononi ambayo ni mkataba wa kuweka mikono juu ya wagonjwa nao watapona ni mkataba wa uponyaji.
Tumepewa mkataba wa kila tutakapokanyaga tumepewa. Usisubiri mtu akutabirie pesa, kanyaga sehemu unayotaka kumiliki. Wachawi wao wana mikataba ya damu ya wanyama sisi tunayo mikataba ya damu ya Yesu.
Abrahamu hakuangalia nchi ile wanakaa watu yeye aliangalia kuwa amepewa tayari na Mungu ashikaye mikataba. Yesu akaenda mbele kidogo akavishwa taji ya miiba kwahiyo damu ya kichwani ikatoka kwahiyo ukawa mkataba umefanyika.
Pale aliposulubiwa Yesu panaitwa kalvari maana yake panaitwa Fuvu la kichwa sababu kichwa cha mtu ni sehemu pekee ambayo milango mitano ya ufahamu inapatikana. Damu ya Yesu ikamwagika kichwani kwahiyo tunao mkataba na Bwana wa kutologwa wal kutoonewa na nguvu za giza, mtu akikuloga anajisumbua sababu unao mkataba.
Mkataba mwingine uliofanyika msalabani, tangu saa sita mpaka saa tisa dunia ikawa giza, makaburi yakafunguka, miamba ikapasuka, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili na baadaye Bwana Yesu akakata roho .Kabla ya kukata roho walienda ili kumkata miguu ili damu imwagike afe haraka ,kabla ya saa tisa wale wezi wawili wakakatwa miguu lakini walipofika Yesu alikuwa ameshakufa.
Damu ya Yesu inazo seli,ule (wekunduwekundu) na maji. Kisayansi mtu akifa damu inajitenga seli na maji kivyake. Sayansi imethibitisha kwamba Yesu alikufa na ile damu iliyomwagika ni damu ya uhai kwamba hatutakufa bali tutaishi, wachawi wakituloga ili tufe damu ya Yesu inazuia mpaka muda uliopangwa ufike.
Yesu alipitisha mikataba ya damu ndipo akafa, alipofufuka alikuja kuisimamia ile mikataba yake aliyoipitisha kwetu.
Mashetani wanaitwa wasimamizi wa mikataba. Agano linaposainiwa na shetani kuna ishara ya mkataba.
Mwanzo 9: 11 “Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata
milele;”
Mungu ameangamiza dunia yote kwa maji na watu wakafa na baadaye akaweka mkataba na Nuhu kwamba hatawaangamiza watu kwa maji na akaweka ishara ya upinde wa mvua. Mkataba huwa ishara.
ALAMA YA CHALE
Ndio maana ukienda kwa mganga wa kienyeji anakuwekea chale kama ishara ya maagano yeno na mashetani yatakapoziona zile ishara yanakumbuka ule mkataba. Chale hizo hazina nguvu bali nyuma yeke yamo mashetani
“Kuanzia leo nafuta chale zote zinazowavuta mashetani wanayosimamia maagano ya damu nazifuta kwa damu ya Yesu maagano ya umaskini, maagano ya magonjwa nazifuta kwa damu ya Yesu.”
ALAMA YA HIRIZI
Hirizi ni alama ya kuwavuta mashetani kwasababu ni alama ya mkataba na mashetani.
PETE ZA BAHATI
Hayo ni maagano ya kichawi ambayo mashetani wanapokuona umeivaa wanasema huyu ni wakwetu
MICHORO YA KWENYE MWILI
Biblia inasema usijichore mwilini mwako hii ni alama ya kuwavuta mashetani unapojichora.
KUNYOA NYWELE KWENYE MISIBA
Wairak, wambulu, wasomali, warwanda, watusi, waethiopia, wasomalia wote wale asili yao ni mesopotania na huko ndiko mila ya kunyoa nywele ilikoanzia. Maana yake ukinyoa nywele kama utakufa kama alivyokufa, maana yake kama alikufa kwa kansa, na wewe utakufa kwa kansa.
KUTUNZA VITOVU
Siku hizi kuna benki ya kitovu .Wanasema zile seli mama zinapatikana kutokea kwenye vitovu hivyo, maana yake hata kama ukija kuugua figo ukiwaendea wale wanakwenda kukuoteshea maabara figo nyingine kuliko kuwekewa nyingine. Kuna watu wengine hata hawajasoma hiyo sayansi lakini wanajua kitovu kinauwezo wa kumshika mtu wanafanya mtu akizaliwa wengine wanatunza kitovu chake yaani unamwona mtu anaishi lakini ni kivuli yeye amewekwa darini au kwenye chungu.
KUOGESHWA NA MGANGA
Unaweza kumkuta mtu ni mkurugenzi anaenda kwa mganga wa kienyeji kuogeshwa ili kuondolewa mikosi, lakini lile ni agano la kichawi ambalo wanakufanya wewe unakuwa wa kwao.
KULA CHAKULA CHA KICHAWI
Unapokwenda kwenye arobaini lazima watu watapandisha mapepo na chakula chao hicho ndicho chakula cha kichawi. Sisi hatuli chakula kwaajili ya wafu bali tunakula chakula kwaajili ya Bwana kwasababu chakula ni sehemu ya Baraka. Alikuwepo Danieli ambaye alikuwa babeli lakini hakula chakula cha Mfalme, aliishi babeli lakini hakutenda mila ya Babeli. Aliishi babeli na akaigusa Babeli kwa mikono mitakatifu. Wao wanakupa chakula ili uharibikiwe zaidi, ili ukataliwe zaidi, ili uugue zaidi.
KUOTA UNA MAHUSIANO NA MTU KICHAWI
Hii ni alama ya kichawi.
Kuna matukio yanaweza kukupata ukatoka damu ili wachawi wapate kufanya mkataba wa damu pamoja na wewe ili wakumiliki kukufanyia chochote kwasababu damu ni uhai. Utakapoivunja hiyo mikataba ya damu hawatakuwa na mkataba na wewe.
“kwa jina la Yesu navunja mikataba ya damu waliotengeneza ili kunimiliki iliyoharibu tumbo la uzazi, iliyoharibu biashara, iliyoharibu elimu, wale mapepo na walisimamia mikataba ikivunjwa wanaondoka, kwa jina la Yesu ninavunja mikataba ya kuharibu biashara, ya kuharibu kwa damu ya Yesu. Mikataba ikivunjwa wasimamizi wanaondoka sababu wanakosa mahali pa kukaa .Amen

Share this:

Post a Comment

 
Copyright © Yote Yanawezekana Kwa Yesu. Designed by OddThemes