Headlines

AKILI YA KIZIJUA NYAKATI

INATUPASA KUWA NA AKILI ZA KUZIJUA NYAKATI 
Wana wa Isakari, walikuwa watu wenye akili za kuzijua nyakati, na kuyajua yawapasayo Israeli wayatende (1 NYAKATI 12:32). Sisi pia, inatupasa kuwa na akili za kujua nyakati, na kuyajua yatupasayo kuyatenda. Tusikubali kuzidiwa akili za kujua nyakati, na ndege wa angani. Tunasoma katika YEREMIA 8:7, "Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui ..." Ndege hawa, koikoi, mbayuwayu, korongo, na aina fulani za hua; hawapendi hali ya hewa ya baridi, bali hufurahia hali ya hewa ya joto. Kwa sababu hii, huko Ulaya, ndege hawa hupatikana kwa wingi, majira ya joto. Wiki kadha, kabla ya majira ya baridi (winter) kuanza, ndege hawa, huwa na akili za kujua kwamba, majira ya baridi karibu yataanza, na hivyo huanza safari ya kuja Afrika, kwenye joto. Kwa mfano, huko Uingereza, korongo huwa wanakuwepo kila mwaka, kuanzia mwezi wa Aprili hadi mwezi wa tisa. Mwezi wa tisa, korongo hawa huanza safari ya kuja Afrika, ili kukwepa majira ya baridi ambayo huanza takribani miezi miwili hivi, baada ya wakati huo. Ndege hawa husafiri mchana tu, na husafiri mwendo wa kilomita 320 kwa siku; na hivyo huchukua wiki sita au zaidi kufika Afrika, kutegemea wanakwenda nchi gani ya Afrika. Kisha tena, wiki kadha kabla ya mwezi wa Aprili, ndege hawa huanza tena safari ya kurudi Uingereza, wakijua kwamba majira ya baridi huko, yanakaribia kwisha.

Sasa basi, Mungu anatarajia kwamba, sisi pia, tutakuwa kama wana wa Isakari, na pia kama ndege hawa; na kuwa na akili ya kuzijua nyakati hizi tunazoishi sasa, na kuyajua yale yanayotupasa kuyatenda, katika majira haya. Tutawezaje kuwa na akili ya kuzijua nyakati hizi? Ni kwa kumwomba Mungu atufunulie akili zetu, ili tupate kuyaelewa maandiko (LUKA 24:45). Maandiko yanasema nini kuhusu nyakati hizi tunazoishi? Biblia inatujulisha kwamba nyakati hizi, ni nyakati za mwisho. Mwana wa Adamu, yaani Yesu Kristo, yuko karibu sana kuja kulinyakua Kanisa, au kuwanyakua watakatifu wake walioko duniani (ZABURI 16:3; WAEBRANIA 10:37; 1 WATHESALONIKE 4:15-17; LUKA 17:34-36). Tunajuaje kwamba, nyakati hizi, ndizo nyakati za kuja kwa Yesu Kristo kulinyakua Kanisa?

Siku au saa ya kuja kwake, hakuna aijuaye (MATHAYO 24:36). Hata hivyo, Yesu Kristo alitufahamisha ishara au dalili nyingi zitakazoashiria kwamba, kuja kwake kumekaribia sana. Nafasi hapa haitoshi, kuziangalia dalili zote alizozitaja Yesu Kristo, zitakazoashiria kwamba, kuja kwake kumekaribia. Hata hivyo, tutaangalia kwa undani hapa, baadhi ya dalili hizo. Akizungumzia dalili hizo, Yesu Kristo alisema katika LUKA 17:26-30, "NA KAMA ILIVYOKUWA SIKU ZA NUHU, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu ...... Na kadhalika, KAMA ILIVYOKUWA KATIKA SIKU ZA LUTU ..... HIVYO NDIVYO ITAKAVYOKUWA SIKU ILE ATAKAYOFUNULIWA MWANA WA ADAMU." Maana yake ni kwamba, muda mfupi kabla ya kuja kwa Yesu Kristo kulinyakua Kanisa, hali iliyoko duniani, itakuwa kama hali ile iliyokuwako nyakati za Nuhu, na nyakati za Lutu. Tuanze kwanza kutafakari juu ya hali iliyokuwako nyakati za Nuhu. Nyakati za Nuhu, inatajwa kwamba, watu walikuwa wakioa na kuolewa (LUKA 17:27). Maana yake ni nini? Kuachana katika ndoa, hali ya kuwa na "michepuko", yaani hali ya uzinzi na uasherati, ilikithiri. Je, hali ya uzinzi na uasherati hivi sasa duniani, ikoje? Inatisha! Ni mbaya zaidi, kuliko nyakati za Nuhu!

Takwimu za hivi karibuni, zinaeleza kwamba, ukahaba umehalalishwa kisheria katika nchi 77 duniani. Kulingana na ripoti ya Shirika la FONDATION SCELLES (via LE FIGARO), makahaba (machangudoa) wanaoishi kwa kuuza miili yao, wako takribani milioni 48 duniani, na wengi wao wanalipa kodi kutokana na kazi "halali" wanayoifanya. Kwa mfano, katika nchi ya Ujerumani, ukahaba ni kazi halali kisheria, inayotozwa kodi; na idadi ya wanawake wanaouza miili yao na kutozwa kodi, katika nchi hiyo, ni zaidi ya 400,000 (laki nne); wanaowahudumia wateja wanaume zaidi ya 1,200,000 (milioni moja na laki mbili), KILA SIKU! Kuna madanguro ya machangudoa kila mahali nchini humo, na danguro kubwa zaidi linaitwa PASCHA, lililoko katika Jiji la Cologne, ambalo ni Jengo la orofa 12, lililosheheni machangudoa. Sekta ya ukahaba nchini Ujerumani, inaingiza pato la Euro bilioni 15 (zaidi ya shilingi za Tanzania, trilioni 38); kwa mwaka!

Nchini Uholanzi, nako pia, madanguro ya machangudoa wanaouza miili yao, na kutozwa kodi na Serikali; yametapakaa kila mahali nchini humo. Katika Jiji la Amsterdam, mji mkuu wa Uholanzi; kuna eneo kubwa linaloitwa "Amsterdam Red Light District" au "De Wallen", ambalo limesheheni madanguro yenye jumla ya machangudoa takribani 4,000. Katikati ya eneo hilo, kuna sanamu kubwa sana ya mwanamke kahaba, inayoitwa "Belle", yenye maandishi makubwa ambayo tafsiri yake Kiswahili, ni, "WAHESHIMU MACHANGUDOA WOTE DUNIANI"!

Tuangalie sasa hali ya ukahaba katika nchi ya Bangladesh. Wakazi wengi wa nchi ya Bangladesh, ni waislamu. Kulingana na takwimu rasmi za nchi hiyo, mwaka 2011, idadi ya waislamu nchini humo, ilikuwa asilimia 90 ya wakazi wote wa nchi hiyo. Hata hivyo, katika nchi hiyo, ukahaba ni halali kisheria. Kuna madanguro mengi mno ya machangudoa, pembe zote za nchi hiyo. Moja kati ya madanguro hayo, ni danguro kubwa sana lililoko kijiji cha DAULATDIA, kilichoko km 100 kutoka Dhaka, mji mkuu wa nchi hiyo. Kijiji chote hiki, ambacho eneo lake ni sawa na takribani viwanja 44 vya mpira wa miguu, wakazi wake wote ni wanawake machangudoa, ambao kazi yao ni moja tu, kuuza miili yao. Katika kijiji hicho, chenye vibanda vingi, kuna machangudoa 2,000 wanaowahudumia wateja wanaume wasiopungua 3,500 kila siku.

Nafasi haitoshi hapa, kuelezea hali ya ukahaba wa jinsi hii, duniani kote. Hata hivyo, ni muhimu pia kufahamu kwamba, vilevile, ziko nchi ambazo, ingawa ukahaba siyo kazi halali kisheria katika nchi hizo, hata hivyo, makahaba hawabughudhiwi na serikali za nchi hizo. Moja kati ya nchi hizo, ni INDIA. Kwa mfano, katika Jiji la Kolkata, nchini humo, iko wilaya inayoitwa SONAGACHI, ambayo takribani wakazi wake wote ni wanawake machangudoa. Jumla ya machangudoa walioko Sonagachi, ni 11,000; ambao nao, kazi yao ni moja tu, kuuza miili yao kila siku; na wanacho chama chao cha ushirika kinachoitwa DMSC, ambacho kazi yake kuu, ni kutetea maslahi yao.

Labda itakuwa vema tumalizie sasa, kwa kuangalia jinsi uzinzi na uasherati ulivyokithiri duniani; kwa kutafakari juu ya ngono inayofanywa katika nyakati hizi, kati ya wanadamu na wanyama. Ngono kati ya wanadamu na wanyama, ni halali kisheria, katika nchi saba duniani: Argentina, Cambodia, Japan, Russia, Finland, Hungary, na Romania; pamoja na takribani majimbo (states) manane ya Marekani. Katika baadhi ya nchi, kuna madanguro maalum ya ngono kati ya wanadamu na wanyama na ndege. Katika madanguro hayo, mtu hulipa fedha ili kufanya ngono na wanyama na ndege; kama vile, mbuzi, kondoo, punda, mbwa, paka, ng'ombe, kuku, bata n.k! Kwa hakika, kizazi hiki ni kizazi cha zinaa, kilicho kibaya zaidi kuliko kizazi cha Nuhu!

Tupige hatua nyingine tena. Tuangalie sasa juu ya nyakati za Lutu. Nyakati za Lutu zilikuwaje? Watu wa nyakati za Lutu, katika miji ya Sodoma na Gomora, walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA (MWANZO 13:13). Nyakati za Lutu, watu walikuwa wachafu sana; ufiraji na ulawiti (1 WAKORINTHO 6:9), ulikithiri kiasi kwamba, watu walitamani kuwalawiti malaika (MWANZO 19:1-11). Dunia ya leo, nayo ikoje? Ndoa za mashoga na wasagaji, zilianza kufungwa na kutambuliwa kisheria, katika ulimwengu huu wa sasa, MIAKA 18 TU ILIYOPITA, yaani mwanzoni tu mwa karne hii; hususan mwaka 2001. Nchi ya kwanza kabisa kuhalalisha kisheria ndoa za mashoga na wasagaji, ilikuwa nchi ya Uholanzi, ambako sheria ya kutambua ndoa hizo, ilianza kutumika tarehe 1 Aprili 2001; na ndani ya dakika ya kwanza tu baada ya siku hiyo kuanza, yaani saa sita usiku; ndoa nne zilifungwa na Meya wa Jiji la Amsterdam, mji mkuu wa Uholanzi; Job Cohen. Hadi sasa, ndoa za mashoga na wasagaji, zinafungwa na kutambuliwa kisheria, katika nchi 28 duniani: Argentina, Australia, Austria, Belgium, Brazil, Canada, Colombia, Denmark, Ecuador, Finland, France, Ujerumani, Iceland, Ireland, Luxembourg, Malta, Mexico, Uholanzi, New Zealand, Norway, Ureno, Afrika Kusini, Spain, Sweden, Taiwan, Uingereza, Marekani na Uruguay. Baadhi ya ndoa hizi, zinafungwa "makanisani". Kwa mfano, huko Denmark, kufikia mwaka 2017, miaka mitano baada ya sheria ya kuhalalisha ndoa hizo nchini humo, kuanza kutumika; zilikuwa tayari zimekwisha kufungwa "makanisani", ndoa 416 za mashoga na wasagaji.

Siyo hilo tu, wako Viongozi wakuu wa nchi kadha duniani, ambao wako madarakani hata hivi sasa; ambao wanaona fahari kujitambulisha hadharani, kwamba, ndoa zao ni za mashoga na wasagaji. Kwa mfano, Waziri Mkuu wa nchi ya LUXEMBOURG, Xavier Bettel; ni mwanaume shoga aliyeoana na mwanaume mwenzake, Gauther Destenay. Vilevile, Waziri Mkuu wa nchi ya IRELAND, Leo Varadkar; ni mwanaume shoga aliyeoana na mwanaume mwenzake, Matthew Barrett. Na pia, Waziri Mkuu wa nchi ya SERBIA, Ana Brnabic; ni mwanamke msagaji aliyeoana na mwanamke mwenzie, Milica Durdic. Mawaziri mashoga na wasagaji, hawa ni wengi zaidi, hata hivyo itoshe kumtaja mmoja hapa. Kwa mara ya kwanza, mwezi wa Juni, mwaka huu wa 2019; nchi ya ISRAELI, imepata Waziri wa kwanza, mwanaume shoga, Amir Ohana; ambaye ni Waziri wa Sheria, wa nchi ya Israeli, aliyeoana na mwanaume mwenzie, Alon Hadad. Siyo hilo tu! Huko Marekani na Canada, kuna maeneo au miji na vijiji vinavyojulikana kama "gay cities" au "gay villages", ambavyo takribani wakazi wake wote, ni mashoga na wasagaji. Hali ya nyakati hizi, ni mbaya zaidi kuliko hali ile ya nyakati za Lutu!

Dalili ya mwisho tunayoiangalia katika somo hili, ambayo pia ni moja ya dalili nyingi nyingine, alizozitaja Yesu Kristo, za siku za mwisho; ni dalili aliyoitaja katika MATHAYO 24:11, "Na manabii WENGI wa uongo watatokea, na kudanganya WENGI." Je, hatuwaoni manabii wengi waliochipuka kama uyoga duniani leo, wanaohubiri Injili ya namna nyingine, badala ya Injili ya Kristo? (WAGALATIA 1:6-9). Badala ya kumhubiri Kristo aliyesulubiwa (1 WAKORINTHO 1:23-24), wao wanahubiri na kuuza maji, keki za upako, mafuta, chumvi, unga, maji, bangili, picha za mhubiri, vijiti vya kuchokonolea meno, mawe, balbu za umeme, sabuni, mifagio, coca cola za upako n.k. Katika ibada zao, hawazungumzi kamwe juu ya kuzaliwa mara ya pili (YOHANA 3:3), wala hawawaambii watu juu ya kutubu dhambi zao na kuziacha (MITHALI 28:13; MATENDO 3:19); na kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana wao (YOHANA 1:12; WARUMI 10:9). Hawataji kamwe juu ya uzima wa milele (YOHANA 3:16; WARUMI 6:23), bali wanataja tu "upako" wa kupata vitu vya dunia hii tu, kinyume na Injili ya Yesu Kristo aliyesema katika MARKO 8:36, "Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?"

Tunapoyaona haya, tuwe na akili za kuzijua nyakati, na kuyajua yatupasayo kuyatenda. Tusikubali kuzidiwa akili na ndege hawa koikoi, hua, mbayuwayu, na korongo; wenye akili za kujua kwamba, majira ya baridi yako karibu kuja. Inatupasa kufahamu kwamba, wakati huu, Yesu Kristo, Kichwa cha Kanisa, analisafisha Kanisa lake kwa maji katika Neno, apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lolote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa (WAEFESO 5:25-27). Mhubiri, inakupasa kukumbuka kwamba Yesu Kristo anafanya kazi pamoja na sisi (1 WAKORINTHO 3:9). Uwe hodari na moyo wa ushujaa, usiogope (YOSHUA 1:9); lihubiri Neno la kweli la utakatifu, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho (2 TIMOTHEO 4:1-5); ukijua kwamba, hakuna mtu yeyote atakayemwona Bwana Yesu, asipokuwa na huo utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Wewe uliyeokoka, acha kuishi maisha ya wokovu vuguvugu, utatapikwa (UFUNUO 3:15-19). Wewe ambaye hujaokoka, wakati uliokubalika wa kuokoka, ni SASA (2 WAKORINTHO 6:2). Usipende tu kuzunguka huku na huko kutafuta miujiza, bali ipende na kuitafuta kweli ya Neno la wokovu. Siku hizi za mwisho, watu ambao wanataka tu miujiza, lakini hawaipendi ile kweli, wapate kuokolewa; Mungu atawaachia nguvu ya upotevu, wauamini uongo wa ishara na ajabu za uongo za Shetani (na manabii wake wa uongo); ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu (2 WATHESALONIKE 2:9-12). Watu ambao hawajaokoka, hawatanyakuliwa, bali watabaki hapa duniani, ambapo kutakuwapo dhiki kubwa ambayo haijatokea namna yake, tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe (MATHAYO 24:21). Tujiweke tayari! (LUKA 12:39-40; AMOSI 4:12). Mwenye masikio, na asikie! (MATHAYO 11:15).
Mwisho
EV.MCHOME
0672870833

Share this:

Post a Comment

 
Copyright © Yote Yanawezekana Kwa Yesu. Designed by OddThemes